Maelfu ya watu wanateseka baada ya kukimbia mapigano katikati mwa Sudan
Takwimu za mamlaka husika zinaonesha kuwa makumi ya maelfu ya watu wanateseka hivi sasa baada ya kukimbia mapigano katika jimbo la Sinnar la katikati mwa Sudan. Watu hao wamekimbilia kwenye jimbo la Gedaref baada ya kushadidi mapigano ya uchu wa madaraka kati ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya RSF na SAF.
Mohamed Adam Mohamed, afisa wa Timu ya Misaada ya Kibinadamu ya Jimbo la Gedaref amesema: "Zaidi ya watu 135,000 wanahangaika hivi sasa baada ya kukimbia mapigano huko Sinnar na kuingia Gedaref. Tumeanzisha makazi ya dharura ya kuwahudumia wakimbizi hao."
Kwa upande wake, Ahmed Al-Amin Adam, waziri wa afya wa Jimbo la Gedaref, amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, mamlaka husika zimeanzisha kituo kikuu cha kupokea watu wanaokimbia mapigano huko Sinnar. Amesema, karibu familia 100 zimeshapewa makazi ya muda katika jimbo hilo.
Wengi wa waliokimbia makazi yao wanalalamikia matatizo wanayokumbana nayo katika vituo walivyowekwa huko Gedaref, ikiwa ni pamoja na uhaba wa maji, uchakavu wa mazingira na uwezekano wa kuenea magonjwa yanayosambazwa na wadudu kama vile mbu na nzi.
Bi Makka Ali, 69, ni miongoni mwa wakimbizi hao ambaye ametokea eneo la Jabal Muya huko Sinnar na kukimbilia katika jimbo la Gedaref kwa miguu kwa muda wa siku tatu. Analalamika akisema: "Tumepoteza kila kitu na tunahitaji kupatiwa msaada wa kuanzia maisha upya."
Mkimbizi mwingine ni Jalila Saeed, ambaye alikimbia kutoka Gezira hadi Sinnar mwezi Disemba mwaka jana na mwaka huu amelazimika kukimbia tena kutoka Sinnar hadi Gedaref kutokana na kuongezeka mapigano baina ya majenerali wa kijeshi huko Sinnar, katikati mwa Sudan.
Tangu Juni 24, mapigano ya silaha yameongezeka sana kati ya Jeshi la Sudan SAF na wapiganaji wa RSF huko Sinnar na kuwalazimisha maelfu ya raia kukimbilia kwenye majimbo mengine ya Gedaref, Kassala na Blue Nile.