Rais Kiir: Uchaguzi Sudan Kusini utafanyika kama ilivyopangwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114148-rais_kiir_uchaguzi_sudan_kusini_utafanyika_kama_ilivyopangwa
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesema kuwa, uchaguzi wa nchi hiyo utafanyika katika muda uliopangwa.
(last modified 2024-07-17T00:37:55+00:00 )
Jul 17, 2024 00:37 UTC
  • Rais Kiir: Uchaguzi Sudan Kusini utafanyika kama ilivyopangwa

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesema kuwa, uchaguzi wa nchi hiyo utafanyika katika muda uliopangwa.

Salva Kiir ameendelea kusisitiza kuwa ni lazima uchaguzi huo ufanyike licha ya kutotekelezwa kikamilifu kwa mkataba wa amani uliofikiwa mwaka 2018.

Sisitizo hilo la Rais Kiir limetolewa ikiwa imebakia miezi mitano kuelekea uchaguzi mkuu wa kwanza tangu Sudan Kusini ilipopata uhuru wake mwaka 2011 na hivyo kujitenga rasmi na Sudan.

Hata hivyo, wanasiasa wa mrengo wa upinzani hasa kutoka chama chake Riek Machar wanaendelea kusisitiza kuwa, kutotekelezwa kwa mkataba wa amani, likiwemo suala la upatikanaji wa katiba mpya ni miongoni mwa mambo ambayo yalipaswa kutangulia uchaguzi huo.

Riek Machar, kiongozi wa upinzani na hasimu wa kisiasa wa Raiis Salva Kiir

 

Licha ya upinzani huo, Rais Salvar Kiir amesisitiza kuwa, pamoja na mapungufu yaliyopo lakini uchaguzi mkuu wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika utafanyika kama ulivyopangwa yaani Disemba 22 mwaka huu.

Vita vya ndani nchini humo vilivyoanza Disemba 2013 vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.