MSF yataka mashirika ya Umoja wa Mataifa kurejea Sudan
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limetoa mwito kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa kurejea Sudan.
Kiongozi wa shirika hilo amesema, Mmshirika ya Umoja wa Mataifa na makundi mengine ya kimataifa ya misaada “ni lazima yarudi na kuwasaidia zaidi wananchi wa Sudan wanaokabiliwa na hali mbaya.”
Mwenyekiti wa MSF International Christos Christou ameziambia duru za habari kwamba, baada ya miezi 15 ya mzozo wa kikatili katika taifa hilo la kaskazini mashariki mwa Afrika, mtu mmoja kati ya watatu wanaojeruhiwa ni wanawake au watoto wenye umri wa chini ya miaka 10.
Vita vilizuka mwezi Aprili mwaka 2023 kati ya jeshi la serikali na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF), na kuitumbukiza Sudan katika “moja ya mizozo mibaya ya kibinadamu katika kumbukumbu za hivi karibuni”, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema njaa imechukua nafasi ya machafuko na kuwa kichochezi kikubwa zaidi cha mawimbi ya watu kuhama kutoka Darfur, ambako kunashuhudiwa vikwazo vingi katika operesheni za utoaji wa misaada ya kibinadamu.
Asasi mbalimbali za kieneo na kimataifa zimekuwa zikitahadharisha kuhusiana na kuzidi kuzorota hali ya kibinadamu nchini Sudan.
Sudan ilitumbulia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 15, 2023 kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) chini ya amri ya Mohammed Hamdan Dagalo.