Al-Tijani Sissi: Makosa ya kipindi cha mpito yameitumbukiza Sudan kwenye vita
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114222-al_tijani_sissi_makosa_ya_kipindi_cha_mpito_yameitumbukiza_sudan_kwenye_vita
Mkuu wa Harakati ya Kitaifa nchini Sudan, Al-Tijani Sissi, amesema makosa makubwa yaliyofanywa katika kipindi cha mpito, ikiwa ni pamoja na kutengwa baadhi ya makundi na matiokeo yake kama pengo lililojitokeza katika jamii ya Sudan, viliitumbukiza Sudan katika vita vya ndani mnamo Aprili 15, 2023.
(last modified 2024-07-19T00:15:05+00:00 )
Jul 19, 2024 00:15 UTC
  • Al-Tijani Sissi: Makosa ya kipindi cha mpito yameitumbukiza Sudan kwenye vita

Mkuu wa Harakati ya Kitaifa nchini Sudan, Al-Tijani Sissi, amesema makosa makubwa yaliyofanywa katika kipindi cha mpito, ikiwa ni pamoja na kutengwa baadhi ya makundi na matiokeo yake kama pengo lililojitokeza katika jamii ya Sudan, viliitumbukiza Sudan katika vita vya ndani mnamo Aprili 15, 2023.

Mkuu wa Harakati ya Kitaifa nchini Sudan ameongeza kwamba, nchi hiyo inakabiliwa na migawanyiko ya kisiasa, kikaumu na kikabila, na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vimetumia vibaya migogoro hiyo.

Al-Tijani Sissi pia amezungumzia nafasi ya nchi za kikanda na athari za ajenda ya kimataifa katika kuchochea mzozo nchini Sudan, na kusema kuwa ufadhili wa nchi za nje ndio sababu kuu ya kuendelea vita hadi sasa, na wapiganaji wa RSF hawataacha kufyatua risasi isipokuwa madola ya kigeni yatakaposimamisha ufadhili ya misaada yao.

Akizungumza kwa huzuni, Mkuu wa Harakati ya Kitaifa nchini Sudan amesema kuwa, suluhisho la mgogoro wa sasa wa Sudan "haliko tena mikononi mwa Wasudani kama ilivyotarajiwa," na inasikitisha kuona kwamba, "kuna uingiliaji mkubwa wa madola ya kigeni unaoelekeza makundi ya ndani ya nchi kwa ajili ya kutimiza malengo ya nchi za kigeni na si kukidhi mahitaji ya Wasudan.”

Hivi karibuni Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilitangaza kwamba zaidi ya Wasudan milioni 10 wamekimbia kutoka miji na vijiji vyao tangu kuanza vita vya ndani mwezi Aprili 2023, huku njaa ikiendelea kuathiri raia wengi wa nchi hiyo.

Sudan

Mwezi uliopita, mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa yaliripoti utabiri mpya wa kutisha kuhusu usalama wa chakula nchini Sudan, yakisema kwamba nchi hiyo inakabiliwa na "janga kubwa la njaa" ambalo halijawahi kutokea tangu mgogoro wa Darfur mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Sudan imetumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya pande mbili zinazoongozwa na majenerali wa jeshi, na juhudi za kusuluhisha hazijazaa matunda hadi sasa.