WHO yasikitishwa na mashambulizi dhidi ya hospitali na vituo vya afya Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114224-who_yasikitishwa_na_mashambulizi_dhidi_ya_hospitali_na_vituo_vya_afya_sudan
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza wasiwasi lilionao kutokana na kuongezeka mashambulio yanayolenga hospitali na vituo vingine vya kutoa huduma za afya nchini Sudan.
(last modified 2024-07-19T00:19:59+00:00 )
Jul 19, 2024 00:19 UTC
  • WHO yasikitishwa na mashambulizi dhidi ya hospitali na vituo vya afya Sudan

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza wasiwasi lilionao kutokana na kuongezeka mashambulio yanayolenga hospitali na vituo vingine vya kutoa huduma za afya nchini Sudan.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya mashariki mwa Mediterania Hanan Balkhy amesema tangu kuanza kwa vita mnamo mwezi April mwaka jana, shirika hilo limeorodhesha mashambulizi 82 yaliyolenga vituo vya afya ikiwa ni pamoja na mashambulizi 17 katika kipindi cha wiki sita za hivi karibuni.

Afisa huyo wa WHO ametahadharisha kuwa nchi hiyo inakabiliwa na hatari ya kuenea kwa magonjwa kama vile kipindupindu, malaria na homa ya uti wa mgongo na kwamba, hujuma na mashambulio dhidi ya hospitali na vituo vya afya yatazidisha kuwa mbaya hali ya utoaji huduma za afya katika nchi hiyo.

Wakati huo huo, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema njaa imechukua nafasi ya machafuko na kuwa kichochezi kikubwa zaidi cha mawimbi ya watu kuhama kutoka Darfur, ambako kunashuhudiwa vikwazo vingi katika operesheni za utoaji wa misaada ya kibinadamu.

Majenerali hasimu wa Sudan ambao wameitumbikiza nchi yao katika vita vya wenyewe kkwa wenyewe

 

Vita vilizuka mwezi Aprili mwaka 2023 kati ya jeshi la serikali na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF), na kuitumbukiza Sudan katika “moja ya mizozo mibaya ya kibinadamu katika kumbukumbu za hivi karibuni”, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Asasi mbalimbali za kieneo na kimataifa zimekuwa zikitahadharisha kuhusiana na kuzidi kuzorota hali ya kibinadamu nchini Sudan.

Sudan ilitumbulia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 15, 2023 kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) chini ya amri ya Mohammed Hamdan Dagalo.