Umoja wa Mataifa walaani kukiukwa haki za binadamu katika magereza CAR
Umoja wa Mataifa umelaani vikali ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika katika magereza ya Jamhuri ya Afrika ya Kati
Umoja wa Mataifa umetoa mwito kwa mamlaka za Jamhuri ya Afrika ya Kati kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha kunakuweko na kuheshimiwa haki za binadamu katika magereza ya nchi hiyo. Ripoti zinaonyesha kuwa, mateso, dhulma, ukandamizaji, kukamatwa watu kiholela na kushikiliwa kizuizini kinyume cha sheria ni jambo la kawaidakabisa nchini humo.
"Maelfu ya watu kwa sasa wanazuiliwa katika jela mbalimbali zilizo na msongamano mkubwa wa watu nchini kote, na upatikanaji mdogo wa chakula, maji, usafi wa mazingira na huduma za afya za kimsingi," inabainisha ripoti hiyo inayozungumzia hali hiyo tangu mwaka wa 2023. Ripoti hiyo inaelezea haswa "tabia ya jeshi na vikosi vya usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kutekeleza operesheni ya kuwakamata watu na kuwaweka kizuizini kinyume cha sheria na kiholela".
Kulingana na Umoja wa Mataifa, mwishoni mwa mwaka 2023, "wafungwa 1,749 walikuwa wakisubiri gerezani kuhukumiwa, wengine kwa karibu miaka sita". "Utapiamlo, ukosefu wa huduma zinazofaa za afya na hali mbaya ya usafi imesababisha uambukizaji wa magonjwa gerezani," unaongeza Umoja wa Mataifa, ambao unasikitishwa na ukosefu wa rasilimali za kutosha zinazotolewa kwa wafungwa.