Indonesia: Tupo tayari kuendelea kuwekeza Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114284-indonesia_tupo_tayari_kuendelea_kuwekeza_tanzania
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo amesema kuwa, Jamhuri ya Indonesia itaendelea kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali.
(last modified 2024-07-20T07:49:21+00:00 )
Jul 20, 2024 07:49 UTC
  • Indonesia: Tupo tayari kuendelea kuwekeza Tanzania

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo amesema kuwa, Jamhuri ya Indonesia itaendelea kuwekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali.

Nyongo amebainisha hayo alipokutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Indonesia, Pahala Mansury ambaye amefanya safari nchini Tanzania kwa ajili ya kuikaribisha Tanzania kwenye Kongamano la Biashara kati ya Indonesia na nchi za Afrika (Indonesia – Africa Forum).

“Ujumbe wa Jamhuri ya Indonesia, ukiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje umefika hapa kwa ajili ya kutualika kwenye Kongamano la Biashara litakalofanyika kuanzia Septemba 1-3, 2024 nchini Indonesia, sisi tumekubali kushiriki Kongamano hilo,” amesema Naibu Wzairi huyo wa nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wa Tanzania.

Aidha amesema,wamejadiliana masuala mbalimbali ikiwemo nchi hiyo ya Indonesia kwenda kuwekeza Tanzania kwenye sekta za uzalishaji wa Kilimo, uzalishaji wa nishati safi, pamoja na uwekezaji kwenye masuala mitandao mbalimbali, Viwanda na Miundombinu.