Uchimbaji madini wasitishwa katika jimbo lenye utajiri wa nishati hiyo huko DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114286-uchimbaji_madini_wasitishwa_katika_jimbo_lenye_utajiri_wa_nishati_hiyo_huko_drc
Mamlaka katika moja ya majimbo yenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imetangaza kusimamishwa kwa shughuli zote za uchimbaji madini ili "kurejesha utaratibu" katika sekta hiyo.
(last modified 2024-07-20T08:05:48+00:00 )
Jul 20, 2024 08:05 UTC
  • Uchimbaji madini wasitishwa katika jimbo lenye utajiri wa nishati hiyo huko DRC

Mamlaka katika moja ya majimbo yenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imetangaza kusimamishwa kwa shughuli zote za uchimbaji madini ili "kurejesha utaratibu" katika sekta hiyo.

Afisa Habari wa jimbo hilo la Kivu ya Kusini Danny Bashige, amesema Gavana wa jimbo hilo Jean-Jacques Purusi "anataka kudhibiti uchimbaji holela wa madini katika eneo hilo." Pasipo kutoa ufafanuziwa taarifa ya Gavana huyo inasema "shughuli za uchimbaji madini zimesitishwa hadi itakapotangazwa tena kwa sababu ya "usumbufu unaosababishwa na waendeshaji madini.”

Uchimbaji madini katika eneo hilo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa muda mrefu umekuwa katika makabiliano ya ghasia kutoka kwa makundi yenye kujihami kwa silaha na usafirishaji wa madini kwenda nchi jirani, kama vile Rwanda.

Mashambulizi kwenye machimbo na vyama vya ushirika vya uchimbaji madini yanatokea mara kwa mara katika eneo hilo ambalo lina makundi zaidi ya 120 yenye kujihami kwa silaha yakishindania ardhi na rasilimali mashariki mwa Kongo.

 

Mapema mwezi huu, wanamgambo walishambulia mgodi wa dhahabu katika mkoa wa Ituri kaskazini mashariki mwa Kongo ambapo waliwaua wachimba migodi sita wa Kichina na wanajeshi wawili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ripoti ya karibuni ya Umoja wa Mataifa imefichua kuwa kati ya wanajeshi 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda wanapigana bega kwa bega na waasi wa kundi la M23 huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huku Kigali ikiongoza pakubwa oparesheni za kundi hilo.