Rais wa Tanzania afanya mabadiliko ya mawaziri, abadilisha mawaziri wawili muhimu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114334-rais_wa_tanzania_afanya_mabadiliko_ya_mawaziri_abadilisha_mawaziri_wawili_muhimu
Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amelifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri na kuwaondoa mawaziri wawili.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jul 21, 2024 23:29 UTC
  • Rais wa Tanzania afanya mabadiliko ya mawaziri, abadilisha mawaziri wawili muhimu

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amelifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri na kuwaondoa mawaziri wawili.

Taarifa yenye saini ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bi Sharifa Nyanga ililyotolewa jana Jumapili imesema kuwa Rais Samia ametengua uteuzi wa mawaziri wawili, Nape Nnauye wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na January Makamba wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mbali na hao, Rais Samia ametengua uteuzi wa Stephen Byabato aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Vile vile Rais Samia amemteua Ridhiwani Kikwete kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) ambaye kabla ya hapo alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Hawa wametemwa, hawamo kwenye baraza jipya la mawaziri la Tanzania

 

Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amechukua nafasi ya Deogratius Ndejembi ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Pia, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameteuliwa kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla ya uteuzi huo, Balozi Kombo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, anachukua nafasi ya January Makamba ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Balozi Kombo anateuliwa kuwa Mbunge ikiwa ni saa chache tangu aliyekuwa Mbunge wa kuteuliwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amuandikie Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson barua ya kujiuzulu ubunge.

Nafasi ya Balozi Mbarouk imechukuliwa na Cosato Chumi aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.