Sudan na Misri zasisitiza msimamo wao kuhusu Bwawa la al-Nahdha
Misri na Sudan zimesisitiza kwa mara nyiingine tena kwamba, misimamo yao kuhusu faili la Bwawa la al-Nahdha ambalo Ethiopia imejenga tangu 2011 kwenye Mto Nile inafanana na haijabadilika.
Ethiopia imejenga bwawa hilo licha ya pingamizi la nchi hizo mbili kwa hatua hiyo na kuzingatia kuwa ni tishio kwa usalama wao wa maji.
Sisitizo hilo limetolewa wakati wa mkutano wa pande mbili mjini Cairo kati ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri Badr Abdelatty na mwenzake wa Sudan Hussein Awad.
Wizara ya Mashauri ya Kigenii ya Misri imesema kuwa, pande hizo mbili zilijadili masuala mbalimbali ya uhusiano wa pande, hali ya Pembe ya Afrika, mzozo wa Ukanda wa Gaza, usalama wa Bahari ya Sham, na hali ya Libya na eneo la Sahel Afrika.
Mwezi Disemba mwaka jana, (2023) mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, ulishuhudia mkutano wa nne na wa mwisho kati ya Ethiopia, Misri na Sudan kuhusu Bwawa la al-Nahdha (Renaissance) linalojengwa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile, ambapo Cairo ilitangaza baadaye katika taarifa ya mwisho kwamba mazungumzo kuhusu bwawa hilo yamegonga mwamba.
Ujenzi wa bwawa hilo umeibua mvutano mkubwa wa maji kati ya nchi hizo tatu tangu mwaka 2011 hadi sasa.
Misri na Sudan zinahofia bwawa hilo kubwa lililogharimu dola bilioni 4.2 litapunguza kwa kiasi kikubwa sehemu ya maji ya Mto Nile wanayopokea, na mara kadhaa zimeiomba Addis Ababa isitishe kulijaza hadi makubaliano yafikiwe.