Wanachama 300 wa Boko Haram wapandishwa kizimbani "kwa mpigo" nchini Nigeria
Kesi ya halaiki ya wanachama 300 wa genge la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram imeanza kusikilizwa kwa mkupuo mmoja nchini Nigeria.
Michael Abu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Kimkakati na Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi cha Nigeria ametoa maelezo kwa ufupi kuhusu mchakato wa kusikilizwa kesi ya watuhumiwa hao.
Amesisitiza kuwa kesi hiyo inachunga viwango vya kimataifa vya haki ya kesi za jinai na inasimamiwa na Mahakama Kuu ya Shirikisho la Nigeria.
Amesisitiza kwamba majaji watano wanasimamia kesi hiyo ili kuhakikisha haki ya haraka inatendeka kuhusu washtakiwa hao 300.
Awali serikali ya Nigeria ilitangaza mipango yake ya kuwafungulia mashitaka wanachama 5,000 wa Boko Haram waliokamatwa katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Magaidi hao wanahukumiwa kwa makundi katika mahakama ya shirikisho.
Tangu mwaka 2009, Boko Haram imekuwa ikifanya na mashambulizi makubwa ya kigaidi nchini Nigeria na kusababisha vifo vya zaidi ya 20,000.
Genge hilo limepanua wigo wa mashambulizi yake hadi nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger tangu mwaka 2015, na kusababisha kuuawa kwa uchache watu 2,000 wengine katika eneo la Bonde la Ziwa Chad.
Mamia kwa maelfu ya Wanigeria huwa wanakimbia makazi yao kila mwaka kutokana na mashambulizi ya kigaidi na migogoro inayoendelea kwenye maeneo yao.