Wimbi la joto kali laua watu 21 nchini Morocco
Vifo 21 vimeripotiwa katika Hospitali ya Mkoa ya Beni Mellàl katikati mwa Morocco kutokana na wimbi la joto kali.
Katika taarifa yake, Wizara ya Afya ya Morocco ilisema kuwa kati ya waliofariki, 17 kulikuwemo wagonjwa ambao walikuwa wanapokea matibabu katika hospitali hiyo.
Wizara hiyo ilibainisha kuwa wengi wa waliopoteza maisha ni wazee na wagonjwa wanaougua magonjwa sugu. Ongezeko kubwa la viwango vya joto liliripotiwa kupelekea hali zao kiafya kuzorota na hatimaye kusababisha vifo vyao.
Mapema Alhamisi, Wizara ya Afya Morocco ilitangaza mipango ya kutekeleza "hatua za haraka za kupunguza athari za wimbi kubwa la joto kwa afya ya watu."
Siku ya Jumapili, Kurugenzi ya Hali ya Hewa ya Morocco ilitoa onyo kwa wananchi, ikitabiri kuwa halijoto inaweza kufikia nyuzijoto 46 katika baadhi ya mikoa kufikia Jumatano. Kurugenzi hiyo iliwataka wakazi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha joto kali. Morocco, nchi ya Afrika Kaskazini yenye hali ya hewa ya
Mediterania, imekuwa ikikabiliwa na hali ya joto inayozidi kuwa ya juu katika miaka ya hivi karibuni.
Kupanda huku kwa halijoto pia kumesababisha ongezeko kueteketa misitu, na kuibua changamoto zaidi kwa taifa.