Burundi yatangaza maambukizo ya kwanza ya MPOX
Waziri wa afya wa Burundi ametangaza kuwa, kumesajiliwa visa vya kwanza vya ugonjwa wa homa ya nyani, Mpox nchini humo, hali ambayo imezusha hofu kwamba kirusi hicho kipya na kikali zaidi kimevuka mpaka na kuingia nchini humo kikotokea nchii jirani.
Taarifa ya Wizara ya Afya iimesema, mamlaka husika nchini Burundi ziliarifiwa mnamo Julai 22 kuhusu "washukiwa" watatu katika hospitali mbili, moja katika wilaya ya wafanyakazi ya mji mkuu wa kiuchumi wa Bujumbura na mwingine nje kidogo ya jiji.
"Vipimo vya sampuli hizo tatu vilibaini kuwepo maambukizi ya Monkeypox," ilisema wizara hiyo, ikiongeza kuwa watu hao watatu "wanaendelea vyema, na orodha ya watu waliowasiliana nao tayari imeundwa na inafuatiliwa".
Majuzi serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilitangaza kuwa, taifa hilo linakabiliwa na "kuongezeka kwa kasi" kwa idadi ya wagonjwa wa Homa ya nyani, Mpox. Msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema kuwa, idadi ya wanaoshukiwa kupata maambukizi ya homa hiyo imefikia watu 11,166, ikiwa ni pamoja na vifo 450.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2022, baada ya mfululizo wa mashauriano na wataalamu wa kimataifa, hatimaye shirika la Afya la Afya Duniani (WHO) lilianza kutumia jina MPOX badala ya Monkeypox au Homa ya Ndui na Homa ya Nyani kwa maelezo ya kwamba lilikuwa linasababisha mambo kadhaa ikiwemo unyanyapaa.
MPOX iligunduliwa kwa mara ya kwanza kwa binadamu katika nchi jirani ya DR Congo mwaka 1970, kulingana na WHO. Kulingana na Shirika la Afya Duniani, tangu mwanzoni mwa Mei 2022, visa vya ugonjwa wa MPOX vimeripotiwa katika nchi ambazo ugonjwa huo si wa kawaida na unaendelea kuenea katika nchi kadhaa.