HRW: Pande hasimu Sudan zimeshiriki katika ukatili mkubwa wa kijinsia
Pande zinazozozana huko Sudan zimeshiriki katika ukatili mkubwa wa kingono na kijinsia katika mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum.
Shirika la Human Rights Watch (HRW) limesema katika ripoti yake leo kuwa wapiganaji wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) na vikosi vya jeshi la Sudan (SAF) mara kwa mara vimekuwa vikitekeleza vitendo vya ubakaji, ubakaji wa magenge na uhalifu mwingine tangu kuanza vita vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Aprili 2023.
Ripoti ya leo ya Human Rights Watch ambayo ni mbali ya ile ya kwanza iliyotaja kushuhudiwa vitendo vya ukatili wa kingono huko Sudan imeandaliwa kwa kutegemea mahojiano na wahudumu wakiwemo wafanyakazi wa vituo vya afya na wafanyakazi wa masuala ya jamii, washauri jamii na wanasheria ambao walizungumza moja kwa moja na mamia ya manusura wa unyanyasaji wa kingono huko Khartoum, na katika miji dada ya Khartoum Kaskazini na Omdurman.
Ripoti ya shirika la HRW imeongeza kuwa: Pande hasimu huko Sudan yaani kikosi cha RSF na jeshi la taifa, zimewatesa wanawake na wasichana wenye umri kuanzia miaka tisa hadi umri usiopungua miaka 60. Wanaume na wavulana pia wamekuwa wahanga wa ukatili wa kingono.
Katika ripoti yake iliyopewa jina la "Vita dhidi ya Mwanadamu - Gharama ya Migogoro na Ukatili nchini Sudan," Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka pia limesema kwamba vikosi vya jeshi la Sudan na vya wapiganaji wa RSF na wafuasi wao vinatenda ukataili wa kutisha kwa watu kote nchini.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, vita vya Sudan vimesababisha kuporomoka kwa ulinzi wa raia, na jamii za wenyeji zinakabiliwa na ukatili wa kiholela, mauaji, mateso na unyanyasaji wa kingono huku mashambulizi yakiendelea dhidi ya wahudumu wa afya na vituo vya matibabu.