DR Kongo: Rwanda Inavuruga GPS na kutekeleza hujuma mtandaoni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114660-dr_kongo_rwanda_inavuruga_gps_na_kutekeleza_hujuma_mtandaoni
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeituhumu nchi jirani ya Rwanda kwa kukwamisha mfumo wa uongozaji kwa satelaiti duniani (GPS) mashariki mwa Kongo na kufanya mashambulizi ya mtandaoni "yenye lengo la uvurugaji".
(last modified 2026-05-10T14:24:40+00:00 )
Jul 30, 2024 23:34 UTC
  • DR Kongo: Rwanda Inavuruga GPS na kutekeleza hujuma mtandaoni

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeituhumu nchi jirani ya Rwanda kwa kukwamisha mfumo wa uongozaji kwa satelaiti duniani (GPS) mashariki mwa Kongo na kufanya mashambulizi ya mtandaoni "yenye lengo la uvurugaji".

Taarifa Wizara ya Mawasiliano ya Kongo DR imesema, uingiliaji huu "hatari" wa GPS unaathiri uelekezaji ndege na hivyo kuhatarisha safari za ndege zinapowasili au kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Goma na maeneo mengine muhimu ya jimbo la Kivu Kaskazini, ikiwa ni pamoja na Beni, Butembo, Kibumba na Kanyabayonga.

Wizara hiyo imesema uchunguzi wa kiufundi uliofanywa na idara husika umethibitisha kuwa uhalifu huo ni kazi ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF).

Rwanda bado haijatoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo.

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulivurugika mwaka 2021 baada ya Kinshasa kuishutumu Kigali kuwa inawaunga mkono waasi wa M23 wanaopigana mashariki mwa nchi hiyo. Kigali inakanusha madai hayo.

Serikali ya DRC imesema imelipeleka suala hilo kwa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), wakala maalumu wa Umoja wa Mataifa unaoratibu kanuni za anga za kimataifa.

Aidha serikali ya DRC imelaani vikali vitendo hivyo ambavyo imesema ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa."