Hujuma ya kigaidi hotelini Mogadishu, watu kadhaa waripotiwa kuuawa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114770-hujuma_ya_kigaidi_hotelini_mogadishu_watu_kadhaa_waripotiwa_kuuawa
Mlipuko na milio ya risasi imetikisa hoteli karibu na ufuo wa bahari katika mji mkuu wa Somalia wa Mogadishu huku watu kadhaa wakiripotiwa kupoteza maisha.
(last modified 2024-08-03T00:56:32+00:00 )
Aug 03, 2024 00:56 UTC
  • Hujuma ya kigaidi hotelini Mogadishu, watu kadhaa waripotiwa kuuawa

Mlipuko na milio ya risasi imetikisa hoteli karibu na ufuo wa bahari katika mji mkuu wa Somalia wa Mogadishu huku watu kadhaa wakiripotiwa kupoteza maisha.

Shirika la Habari la Kitaifa la Somalia linalomilikiwa na serikali limesema vikosi vya usalama "vimewamaliza washambuliaji."

Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa zaidi ya watu kumi wameuawa. Kundi la kigaidi la Al Shabab linalofungamana na Al-Qaeda, limesema kupitia redio yake kwamba wapiganaji wake ndio wametekeleza shambulio hilo.

Ufukwe wa Lido, ni eneo maarufu mjini Mogadishu, na huwa na msongamano mkubwa wa watu siku za Ijumaa usiku.

Eneo la Lido Beach limekuwa likilengwa na wanamgambo wanaoshirikiana na Al-Shabab. Shambulio la mwaka jana lilipelekea watu tisa kuuawa.

Kundi la kigaidi la al-Shabaab limeongeza mashambulizi pamoja na kuwa Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud ametangaza "vita vya kila namna" dhidi ya genge hilo.

Hivi sasa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kinaendelea na mchakato wa kuondoa askari wake nchini humo ili kukabidhi masuala yote ya ulinzi kwa vikosi vya serikali ya Somalia.