UN: Eneo la Darfur Kaskazini nchini Sudan limekumbwa na baa la njaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114772-un_eneo_la_darfur_kaskazini_nchini_sudan_limekumbwa_na_baa_la_njaa
Hatimaye imedhihirika kuwa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan linasumbuliwa na baa la njaa, imesema Kamati ya Tathmini ya Njaa inayohusisha mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau.
(last modified 2024-08-03T00:56:41+00:00 )
Aug 03, 2024 00:56 UTC
  • UN: Eneo la Darfur Kaskazini nchini Sudan limekumbwa na baa la njaa

Hatimaye imedhihirika kuwa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan linasumbuliwa na baa la njaa, imesema Kamati ya Tathmini ya Njaa inayohusisha mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau.

Taarifa inasema mapigano yaliyoshahidi nchini Sudan, ambayo yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya miezi 15 sasa, yamesitisha kwa kiasi kikubwa ufikiaji wa msaada wa kibinadamu na kulitumbukiza eneo la Darfur Kaskazini kwenye baa la njaa.

Kwa mujibu wa tathimini hiyo, “eneo linatajwa kuwa na baa la njaa pindi mtu mmoja kati ya 5 kwenye familia hana chakula, anakabiliwa na njaa, maskini kupindukia na hivyo kukabiliwa na utapiamlo uliokithiri au kifo.”

Kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam imeathiriwa zaidi na iko takriban kilomita 12 kusini mwa mji wa El Fasher. Kambi hiyo ni mojawapo ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi wa ndani (IDP) nchini Sudan, ikiwa na takriban ya wakazi wasiopungua 500,000.

Umoja wa Mataifa umesema: “Kiwango cha uharibifu unaosababishwa na ghasia zinazozidi kuongezeka katika mji wa El Fasher ni kikubwa na cha kutisha. Mapigano yanayoendelea, ni makubwa na yamewalazimisha wakazi wengi kutafuta hifadhi katika kambi za wakimbizi wa ndani ambako wanakabiliwa na matatizo mengi, huduma za msingi ni chache au hazipo, na hivyo kuzidisha ugumu wa watu kuhama makazi yao."

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban watu 320,000 wanaaminika kuwa wamekimbia makazi yao tangu katikati ya mwezi wa Aprili huko El Fasher.

Takriban 150,000 hadi 200,000 kati yao wanaaminika kuhamia kambi ya Zamzam kutafuta usalama, huduma za msingi, na chakula tangu katikati ya Mei na idadi ya watu katika kambi hiyo imeongezeka hadi zaidi ya nusu milioni katika wiki chache.

Pia imeelezwa kuwa vikwazo vya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya makusudi vilivyowekwa na pande zinazohusika kwenye mzozo, vimezuia kwa kiasi kikubwa uwezo wa mashirika ya misaada ya kibinadamu kuongeza juhudi zao za kukabiliana na changamoto kwa ufanisi. Vikwazo hivi vimezuia sana utoaji wa misaada muhimu, kuzidisha changamoto ya chakula na kusababisha baadhi ya kaya kujikuta katika hali ya njaa.