Malawi yachapisha ratiba ya uchaguzi mkuu wa 2025
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114790-malawi_yachapisha_ratiba_ya_uchaguzi_mkuu_wa_2025
Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) jana Ijumaa ilichapisha ratiba ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ambao umepangwa kufanyika Septemba 16, 2025. Ratiba hiyo imetangazwa huko Lilongwe, mji mkuu wa Malawi.
(last modified 2024-08-03T07:22:19+00:00 )
Aug 03, 2024 07:22 UTC
  • Malawi yachapisha ratiba ya uchaguzi mkuu wa 2025

Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) jana Ijumaa ilichapisha ratiba ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ambao umepangwa kufanyika Septemba 16, 2025. Ratiba hiyo imetangazwa huko Lilongwe, mji mkuu wa Malawi.

Mwenyekiti wa MEC, Jaji Annabel Mtalimanja amesema kuwa tume yake itafanya zoezi la uandikishaji wapiga kura kuanzia mwezi Septemba hadi Disemba mwaka huu katika awamu tatu za siku 14-14 kote nchini humo.

Amesema kuwa, kwa sasa, tume hiyo inashirikiana na Ofisi ya Taifa ya Usajili wa Vitambulisho ya Malawi (NRB), ili kuhakiksha kuwa, kila raia wa Malawi mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea, au chini ya miaka 18, lakini atakuwa amefikia miaka 18 ifikapo siku ya uchaguzi, anapata kitambulisho cha taifa.

Amesisitiza kuwa, ingawa katika hatua za juu ni raia wa Malawi pekee ndio wenye haki ya kuwa na kitambulisho cha taifa cha nchi hiyo lakini raia wa kigeni ambao wamekaa nchini humo kwa miaka saba mfululizo, wataoruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa, ubunge na urais wa mwaka 2025.

Amesema kuwa, kuanzia Agosti 6, tume yake itaanza kupokea majina ya waangalizi wa uchaguzi kutoka vyama vya siasa vitakavyoshiriki kwenye kinyang'anyiro hicho.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Malawi itatangaza ada watakazotozwa wagombea wakati wa kujiandikisha na kwamba karatasi za uteuzi wa wagombea wa serikali za mitaa, ubunge na urais zitatolewa katika miezi ya Aprili, Mei na Juni mfululizo.