Rais wa Nigeria atoa mwito wa kukomeshwa maandamano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114834-rais_wa_nigeria_atoa_mwito_wa_kukomeshwa_maandamano
Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu ametoa wito wa kusitishwa kwa maandamano ya nchi nzima na kukomesha "umwagaji damu" baada ya vikosi vya usalama kukabiliana na maandamano ya kupinga hali ngumu ya kiuchumi.
(last modified 2024-08-04T09:02:31+00:00 )
Aug 04, 2024 09:02 UTC
  • Rais wa Nigeria atoa mwito wa kukomeshwa maandamano

Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu ametoa wito wa kusitishwa kwa maandamano ya nchi nzima na kukomesha "umwagaji damu" baada ya vikosi vya usalama kukabiliana na maandamano ya kupinga hali ngumu ya kiuchumi.

Katika hotuba kupita televisheni, Tinubu amewataka waandamanaji kusimamisha maandamano na kutoa nafasi ya mazungumzo, ikiwa ni kauli yake ya kwanza kwa umma tangu maandamano hayo yalipoanza siku ya Alkhamisi.

Katika hotuba hiyo alionesha kuwa amesikia kilio cha wananchi, kuelewa machungu waliyonayo na mfadhaiko uliosababisha waandamanaji na hivyo kutoa ahadi ya serikali kushughulikia kero zao.

Wanigeria waliandamana mjini Abuja, mji mkuu wa kibiashara, Lagos na miji mingine kadhaa kuonyesha kutoridhika na mageuzi ya kiuchumi ambayo yamesababisha mfumuko wa bei uliokithiri na kusababisha matatizo kwa Wanigeria wa kawaida. Rais Bola Tinubu ameapa kuendeleza mabadiliko ambayo anasema yanahitajika ili kuiweka nchi sawa.

 

Takriban waandamanaji watatu wameuawa katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria siku ya Alhamisi, katika maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha na utawala mbovu.

Wakichochewa na maandamano nchini Kenya mwezi Juni yaliyopelekea serikali kufutilia mbali nyongeza ya kodi, Wanigeria wanataka serikali irejeshe ruzuku za petroli na umeme, elimu ya bure ya msingi na upili na kuchukua hatua za kukabiliana na ukosefu wa usalama.

Juma lililopita maelfu ya waandamanaji walianza kuingia barabarani kupinga sera za serikali na gharama kubwa ya maisha. Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeshutumu vikosi vya usalama kwa kuwaua takriban waandamanaji 13, huku polisi wakisema watu saba tu ndio waliofariki na kukana kuhusika na mauaji hayo.