Mali yakata uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine baada ya shambulio la kigaidi
Mali imetangaza kuwa inakata uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine baada ya Kiev kukiri kuhusika katika shambulio la kigaidi la hivi karibuni katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Msemaji wa Serikali ya Mpito ya Mali, Kanali Abdoulaye Maiga amesema katika taarifa yake kuwa serikali hiyo imegundua, kwa mshtuko mkubwa, matamshi ya kushangaza yaliyotolewa na Andriy Yusov, msemaji wa Shirika la Ujasusi la Kijeshi la Ukraine akikiri kuhusika nchi hiyo katika shambulio la woga, la kihaini na la kinyama lililofanywa na makundi ya kigaidi yenye silaha na kuuwa maajenti na askari usalama wa Mali huko Tinzaouaten. Shambulizi hilo limesababisha uharibifu wa mali.
Jeshi la Mali limekiri leo Jumatatu kwamba idadi kubwa ya watu wameuawa kufuatia mapigano yaliyojiri katika eneo la Tinzaouaten, kaskazini mwa nchi hiyo, huku kundi la wanamgambo la Wagner lenye mfungamano na Russia linalolisaidia jeshi la Mali, likithibitisha kuuliwa kamanda wao katika mapigano makali katika eneo hilo.
"Shutuma hizi nzito, ambazo hazijakanushwa, zinaonyesha uungaji mkono rasmi wa serikali ya Ukraine kwa ugaidi barani Afrika, katika eneo la Sahel, na zaidi katika nchi ya Mali," amesema Kanali Abdoulaye Maiga.