Rais wa Uganda apinga vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11494-rais_wa_uganda_apinga_vikwazo_vya_silaha_dhidi_ya_sudan_kusini
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amepinga mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuiwekea Sudan Kusini vikwazo vya silaha na kusema hatua hiyo italidhoofisha jeshi la nchi hiyo ambalo linakabiliana machafuko mapya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 18, 2016 09:37 UTC
  • Rais wa Uganda apinga vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan Kusini

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amepinga mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuiwekea Sudan Kusini vikwazo vya silaha na kusema hatua hiyo italidhoofisha jeshi la nchi hiyo ambalo linakabiliana machafuko mapya.

Kauli ya Museveni imekuja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kulitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea Sudan Kusini vikwazo vya silaha ili kumaliza vita vya miaka miwili katika nchi hiyo changa zaidi duniani.

Karibu watu 272 waliuawa katika mapignao ya siku chache zilizopita baina ya makundi mawili ya Jeshi la Sudan Kusini ambapo kundi moja linamuunga mkono Rais Salva Kiir na jingine, hasimu wake, Makamu wa Rais Riek Machar.

Museveni alitoa kauli hiyo Jumamosi mjini Kigali, Rwanda wakati alipofanya mazungumzo na Ban pembizoni mwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika.

Taarifa ya ofisi ya Museveni imesema, iwapo Sudan Kusini itawekewa vikwazo vya silaha, basi jeshi litadhoofika. Uganda ilituma wanajeshi wake Sudan Kusini kumuunga mkono Salva Kiir kufuatia mapigano yaliyoibuka nchini humo mwaka 2013. Vikosi hivyo viliondoka nchini humo lakini vimerejea tena mwezi huu kufuatia kuibuka mapignao mapya, serikali ya Kampala inasema imetuma askari Sudan Kusini kuwaokoa raia wake.

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 lakini tokea wakati huo nchi hiyo haijashuhudia amani kutokana na malumbano baina ya wanasiasa na makabila makubwa nchini humo ya Nuer na Dinka.