Rais wa Tunisia amfuta kazi Waziri Mkuu na kuteua mpya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114982-rais_wa_tunisia_amfuta_kazi_waziri_mkuu_na_kuteua_mpya
Rais Kais Saied wa Tunisia amemteua Waziri wa Masuala ya Kijamii, Kamel Maddouri kuwa Waziri Mkuu mpya, ili kuchukua nafasi ya Ahmed Hachani, Waziri Mkuu aliyefutwa kazi na rais huyo.
(last modified 2024-08-08T07:10:13+00:00 )
Aug 08, 2024 07:10 UTC
  • Rais wa Tunisia amfuta kazi Waziri Mkuu na kuteua mpya

Rais Kais Saied wa Tunisia amemteua Waziri wa Masuala ya Kijamii, Kamel Maddouri kuwa Waziri Mkuu mpya, ili kuchukua nafasi ya Ahmed Hachani, Waziri Mkuu aliyefutwa kazi na rais huyo.

Ofisi ya Rais wa Tunisia haikutoa maelezo zaidi kuhusu uamuzi huo. Hatua hiyo imechukuliwa miezi miwili kabla ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Oktoba 6. Kais Saied atagombea kwa muhula wa pili wa urais wa miaka mitano mitano.

Waziri Mkuu mpya wa Tunisia, Kamel Maddouri alizaliwa mwaka wa 1974. Aliteuliwa kuwa waziri wa masuala ya kijamii Mei 25, 2024, wakati wa mabadiliko ya serikali. Kabla ya hapo, alikuwa mwenyekiti wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wa Tunisia.

Kabla ya kuteuliwa Maddouri, Rais wa Tunisia alikuwa amemfuta Waziri Mkuu Ahmed Hachani jana Jumatano na baadaye taarifa ya Ikulu ikasema kuwa, Saied amemteua Maddouri kushikama nafasi ya Hachani bila ya kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu usababu za kufutwa kazi Hachani.

Hachani aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tunisia mwezi Agosti mwaka jana.

Rais Kais Saied wa Tunisia

 

Kuachishwa kazi huko kumetokea baada ya kuweko malalamiko mengi ya wananchi ya kutoridhishwa na utendaji kazi wake hasa katika masuala kama ya kukosekana maji na umeme nchi nzima ya Tunisia.

Serikali ya Hachani ilidai kuwa masuala haya yametokana na ukame unaoendelea huko Tunisia na kusababisha kuchukuliwa hatua za kutoa maji kwa mgao. 

Wizara ya Kilimo ya Tunisia inasema kuwa, kiwango cha maji katika mabwawa kiko chini sana kwa asilimia 25. Lakini Rais Saied anadai kuwa uhaba huo wa maji ni njama inayofanywa na wapinzani wake wakati huu wa kukaribia uchaguzi wa rais akisisitiza kuwa mabwawa hayo yana maji ya kutosha.

Saied alitangaza nia yake ya kugombea tena urais mwezi Oktoba mwaka huu. Anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wapinzani, mashirika ya haki za binadamu na wagombea wengine ambao wanamshurumuu kwa kuwakandamiza wapinzani wake ili ashinde katika uchaguzi ujao.