Kituo cha Utafiti: Haya ndiyo mambo yanayoimarisha ugaidi barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i114986-kituo_cha_utafiti_haya_ndiyo_mambo_yanayoimarisha_ugaidi_barani_afrika
Kituo kimoja cha utafiti wa kiistratijia kimesema kuwa, magenge ya kigaidi yamepanua shughuli zao katika ukanda wa Sahel Afrika kwenye miezi ya hivi karibuni, na hali hii inatarajiwa kuongezeka katika miezi ijayo.
(last modified 2024-08-08T07:11:03+00:00 )
Aug 08, 2024 07:11 UTC
  • Kituo cha Utafiti: Haya ndiyo mambo yanayoimarisha ugaidi barani Afrika

Kituo kimoja cha utafiti wa kiistratijia kimesema kuwa, magenge ya kigaidi yamepanua shughuli zao katika ukanda wa Sahel Afrika kwenye miezi ya hivi karibuni, na hali hii inatarajiwa kuongezeka katika miezi ijayo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati cha "Ab'ad" cha nchini Iran kimesema kwenye ripoti yake kwamba vitendo vya magenge ya kigaidi katika nchi za ukanda wa Sahel Afrika vimeongezeka kwenye miezi ya hivi karibuni hususan katika kipindi cha miezi miwili ya Aprili na Mei 2024 na hasa kwenye nchi za Burkina Faso, Mali na Nigeria.

Mwezi uliopita wa Mei, genge moja la kigaidi lilitangaza kuhusika katika mashambulizi 50 ya kigaidi dhidi ya vikosi vya jeshi la Mali na Burkina Faso, wakati genge jingine la kigaidi lenye mafungamano na Daesh (ISIS) limetishia kufanya operesheni zaidi za kigaidi. Kwa mujibu wa kituo cha Ab'ad, katika miezi ijayo nchi za Sahel Afrika zitashuhudia mashambulizi zaidi ya magenge ya kigaidi ambayo nchi hizo zinazishutumu nchi za Magharibi hasa Marekani na Ufaransa kuwa ndizo zinazoyafadhili magenge hayo. 

Uchunguzi wa kituo hicho unasema kuwa, genge la kigaidi la Jabhat al-Nusra ni miongoni mwa wasababishaji wa ukosefu wa amani na kuongezeka vitendo vya kigaidi katika eneo hilo tangu mwaka 2020. 

Kwa mujibu wa kituo hicho, udhaifu wa vikosi vya usalama vya kikanda umesababisha kutokea mapinduzi mengi ya kijeshi katika miaka ya huko nyuma na hiyo ni sababu nyingine ya ukosefu wa usalama katika ukanda huo. Sababu nyingine ni kuwepo vikosi vya madola ya kibeberu hasa Marekani na Ufaransa katika eneo la Sahel Afrika ambavyo vinashutumiwa kwa kusaidia magenge ya kigaidi kinyume kabisa na madai yao ya kulinda usalama.