WHO: Vita vimefanya tuluthi 2 ya Wasudan washindwe kutafuta matibabu
(last modified Fri, 09 Aug 2024 07:18:50 GMT )
Aug 09, 2024 07:18 UTC
  • WHO: Vita vimefanya tuluthi 2 ya Wasudan washindwe kutafuta matibabu

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema thuluthi mbili ya wananchi wote wa Sudan hawawezi kutafuta huduma za matibabu kutokana na mgogoro na vita vinavyoendelea kushuhudiwa nchini humo.

Tedros Adhanom Ghebreyesus amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema hayo na kueleza kuwa, "Theluthi mbili ya watu nchini Sudan hawawezi kwenda hospitali au kuona daktari kutokana na mzozo unaoendelea."

Ghebreyesus amesema hayo kwenye ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa, "Zaidi ya hayo, maelfu ya watu wanakabiliwa na njaa."

Dakta Ghebreyesus ametilia mkazo ombi la Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) kwa Baraza la Usalama la umoja huo kusaidia kutafuta suluhu ya amani na ya kudumu kwa watu wa Sudan.

Wakati huo huo, muungano wa madaktari nchini Sudan umesema kuwa, mji wa El Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur Kaskazini la magharibi mwa nchi hiyo, umegeuka na kuwa mahali hatari zaidi na pabaya zaidi kuishi binadamu duniani kutokana na vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi.

Dakta Ghebreyesus

Kamati Kuu ya Muungano wa Madaktari wa Sudan imesema hayo katika ripoti yake na kuongeza kuwa: "Wakazi wote wa El Fasher wanaweza kufa, imma kutokana na njaa, kiu, risasi, ukosefu wa huduma za afya na matibabu, au kutokana na madhara mengine ya vita vinavyoendelea."

Tangu mapigano kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF yaanze Aprili mwaka 2023, takriban watu 18,800 wameuawa, huku wengine karibu milioni 10 wakilazimika kukimbia makazi yao. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za UN.