Mapigano mapya yaibuka kati ya makundi hasimu mashariki mwa Tripoli, Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115048-mapigano_mapya_yaibuka_kati_ya_makundi_hasimu_mashariki_mwa_tripoli_libya
Watu tisa wameuawa katika mapigano yaliyotokea jana Ijumaa kati ya makundi hasimu katika kitongoji cha Tajoura, mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.
(last modified 2024-08-10T03:55:58+00:00 )
Aug 10, 2024 03:55 UTC
  • Mapigano mapya yaibuka kati ya makundi hasimu mashariki mwa Tripoli, Libya

Watu tisa wameuawa katika mapigano yaliyotokea jana Ijumaa kati ya makundi hasimu katika kitongoji cha Tajoura, mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Huduma ya Ambulensi na Masuala ya Dharura imethibitisha katika taarifa yake kwamba "watu 9 wameuawa  katika mapigano hayo mapya ya mashariki mwa Tripoli."

Taarifa ya Kurugenzi ya Usalama ya Tripoli imesema: "Mapigano hayo yalitokea kati ya wapiganaji wa kikosi cha Rahbat al-Duru' na wanachama wa kikosi cha Shahida Sabria baada ya hitilafu na mzozo ambao uliibuka na kuwa makabiliano ya silaha.”

Wakati huo huo chanzo kimoja ambacho kimeomba kutotajwa jina kimesema kwamba sababu ya mapigano hayo ni kwamba kamanda wa Kikosi cha Rahbat al-Duru’, Bashir Khalaf Allah, alikabiliwa na jaribio la kumuua, bila ya kutoa ufafanuzi zaidi.

Mapigano haya yaliambatana na harakati za kijeshi kusini-magharibi mwa Libya, zilizofanywa na vikosi vya Meja Jenerali mstaafu Khalifa Haftar, mkabala wa "kuondolewa hali ya hatari na dharura" iliyokuwa imetangazwa na vikosi vinavyoitii serikali ya Tripoli.

Libya ilitumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa kisiasa, kiusalama, kiuchumi na kadhalika baada ya madola ya Magharibi, chini ya jumuiya ya kijeshi ya NATO, kuivamia kijeshi nchi hiyo na kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu na baadaye kuitelekeza na kuacha silaha zikiwa zimeenea mikononi mwa makundi hasimu baada ya kupinduliwa utawala wa Kanali Muammar Gadafi.