Aug 21, 2024 11:53 UTC
  • Imam wa Ghana: Arubaini ni nembo ya haki na kupinga dhulma

Msomi mmoja mashuhuri wa Kiislamu nchini Ghana amesema matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS katika mji mtukufu wa Karbala nchini Iraq ni nembo ya mapambano ya haki na kusimama kidete dhidi ya dhulma na maonevu.

Sheikh Mujeeb Muhammed, Naibu Imam wa Msikiti wa Tafo katika jimbo la Ashanti nchini Ghana amesema hayo katika mahojiano maalumu na shirika la habari la Iran Press, ambapo amesisitizia umuhimu wa matembezi ya Arubaini yanayowakusanya pamoja mamilioni ya Waislamu huko Iraq kila mwaka.

Sheikh Mujeeb Muhammed amesisitiza kwamba, mkusanyiko wa Arubaini ya Imam Hussein AS unaashiria dhabihu ya mwisho katika mapambano kati ya haki na udhalimu na ukandamizaji.

Mwanachuoni huyo wa madhehebu ya Sunni nchini Ghana anaitakidi kuwa, Arubaini imejengwa juu ya falsafa ya kupinga dhulma na ukandamizaji, falsafa ambayo ilijengwa juu ya kanuni ya "Usijihusishe na dhulma na usikubali kudhulumiwa pia, na unapasa kupinga ukandamizaji wa aina zote."

Amebainisha kuwa, kutokana na falsafa hiyo, haishangazi kuona katika zama hizi, ni wafuasi wa Imam Hussein AS ambao wanasimama dhidi ya mabeberu wa ulimwengu huu, akiashiria dhulma dhidi ya Palestina na mauaji ya kikatili yanayoendelea kufanywa na utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7, 2023.

Kwa mujibu wa duru za Iraq, watu milioni 22 walishiriki katika kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein (AS) mwaka jana katika mji wa Karbala na kwamba, mwaka huu idadi hiyo inakadiriwa kuongezeka kwa asilimia kumi.

Tags