Umoja wa Mataifa waonya kuhusu hatari kubwa ya mafuriko nchini Somalia
Shirika moja la Umoja wa Mataifa limeonya kuhusu hatari kubwa ya mafuriko nchini Somalia na kusema kuwa, jamii kadhaa nchini humo ziko hatarini kukumbwa na mafuriko huku mito ikiendelea kujaa maji katikati mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Utabiri huo umo kwenye makadirio ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa na Usimamizi wa Taarifa za Maji na Ardhi ya Somalia (FAO-SWALIM) ambayo yanaonyesha kuweko hatari kubwa ya mito kufurika licha ya kuweko ukame wa mvua nchini Somalia na maeneo ya mashariki mwa Ethiopia.
Taarifa ya shirika hilo imesema, kuendelea kutiririka maji kutoka maeneo ya juu nchini Ethiopia kumesababisha kupanda viwango vya maji kandokando ya Mto Shabelle nchini Somalia.
Shirika la FAO-SWALIM pia limetoa mwito wa kuanzishwa mipango ya uokoaji, likionya kwamba kuna hatari kubwa ya mito kufurika katika wilaya za Beledweyne, Bulo Burte, Jalalaqsi, Jowhar, na Balcad na maeneo mengine yanayozunguka wilaya hizo.
Shirika hilo pia limewataka wakazi wanaoishi kando ya maeneo ya mafuriko, hasa katika wilaya za Beledweyne na Bulo Burte, kuwa waangalifu.
Vilevile limezitaka serikali za mitaa na kata kufuatilia kwa karibu hali hiyo na kuchukua hatua za kukabiliana na mafuriko yanayoweza kutokea.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Somalia ilikumbwa na ukame mbaya zaidi mwaka 2023, uliofuatiwa na mafuriko makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini humo ndani ya kipindi cha miezi michache tu.
Idadi ya watu walioathiriwa na mafuriko mwaka 2023 nchini Somalia inakadiriwa kuwa ni milioni 2.48 na takriban watu 118 walifariki dunia mwaka huo.