Mapigano yaibuka tena kati ya jeshi la DRC na waasi wa M23
Mapigano mapya yanaripotiwa kuibuka kati ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi wa M23.
Mapigano hayo yalianza tena hapo jana karibu na mji wenye wakazi wengi mashariki mwa jimbo la Kivu Kaskazini, ambako waasi wanaendesha shughuli zao.
M23 waliteka mji wa Kirumba, kitovu cha kiuchumi cha eneo la Lubero nchini Congo, mwishoni mwa mwezi Juni. Pia waliteka mji jirani wa Kanyabayonga.
Msemaji wa kuundi la M23 Willy Ngoma amesema vikosi vya serikali vilishambulia maeneo kadhaa ya waasi karibu na Kirumba mapema Jumapili asubuhi na kwamba mapigano yanaendelea.
Jeshi katika taarifa yake liliripoti mapigano na M23 katika kijiji cha Kikuvo, takriban kilomita zaidi ya kumi kutoka Kirumba.
Mapigano makali kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali ya Kongo likishirikiana na wanajeshi wa Kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC yamesababisha wimbi jipya la wakimbizi wa ndani mashariki mwa DRC.
Mwezi Januari mwaka huu Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza kuanzisha operesheni ya pamoja na wanajeshi wa kikosi cha Jumuiya ya Maendelezo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC dhidi ya waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo.
Kongo DR imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.