Senegal yasitisha kwa muda uchimbaji madini kwenye mpaka wake na Mali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115750-senegal_yasitisha_kwa_muda_uchimbaji_madini_kwenye_mpaka_wake_na_mali
Serikali ya Senegal imetangaza kuwa, imesimamisha kwa muda wa miaka mitatu shughuli za uchimbaji madini kwenye ukingo wa mto ambao ni sehemu ya mpaka wake wa kusini mashariki na Mali, kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kulinda afya ya wenyeji.
(last modified 2024-08-28T11:51:32+00:00 )
Aug 28, 2024 11:51 UTC
  • Senegal yasitisha kwa muda uchimbaji madini kwenye mpaka wake na Mali

Serikali ya Senegal imetangaza kuwa, imesimamisha kwa muda wa miaka mitatu shughuli za uchimbaji madini kwenye ukingo wa mto ambao ni sehemu ya mpaka wake wa kusini mashariki na Mali, kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kulinda afya ya wenyeji.

Mto Faleme, ukingo mkuu wa Mto Senegal, unakabiliwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira na matumizi makubwa ya kemikali katika migodi ya dhahabu ambayo imekuwa mingi katika eneo hilo.

“Hali hii inayotia wasiwasi inahitaji hatua madhubuti kwa upande wa mamlaka za kitaifa kutafuta suluhu la haki kwa malalamiko yasiyoisha kutoka kwa watu wanaoishi kando ya mto”, wizara ya madini ilisema katika ripoti wiki iliyopita.

Kusimamishwa kwa shughuli hizo kwa miaka mitatu, hatua ambayo itatekelezwa hadi tarehe 30 Juni, mwaka 2027, inahusu eneo la mita 500, kando ya ukingo wa kushoto wa mto Faleme, kulingana na amri ya rais iliyochapishwa Jumanne.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Serikali ya Senegal ilitangaza kuwa, itaangalia upya mikataba ya mafuta na gesi iliyotiwa saini na mataifa mbalimbali.

Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye alisisitiza kwamba, nchi yake inapanga kutathmini na kujadili upya mikataba yake ya mafuta.

 

Kiongozi huyo wa Senegal aliyeshinda urais katika uchaguzi wa mwezi Machi mwaka huu, aliagiza ukaguzi ufanyike katika sekta za mafuta na gesi baada ya kuingia madarakani.

Aidha amebainisha kuwa, majadiliano mapya ya mikataba hiyo yanalenga kuleta manufaa kwa pande zote zinazohusika na mikataba hiyo.

Kwa mujibu wa serikali mpya ya Senegal chini ya uongozi wa Rais Faye, kuna mikataba katika sekta ya mafuta na gesi ambayo inahatarisha maslahi ya taifa na rasilimali za nchi hiyo.