Aug 29, 2024 07:20 UTC
  • Maporomoko ya ardhi yanatishia watu 400,000 kaskazini mwa Ethiopia

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo la kaskazini la Amhara nchini Ethiopia zimewaweka watu 400,000 katika hatari ya mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Tesfaw Batable, Kamishna wa Tume ya Kikanda ya Kuzuia Maafa na Majanga ya Kimaumbile ya Ethiopia ameiambia televisheni ya jimbo la Amhara kuwa wilaya 32 zinakabiliwa na ongezeko la hatari ya kuathiriwa na majanga ya kimaubile kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Batable ametahadharisha kuwa hali ni mbaya, hasa katika maeneo ya Gondar Kaskazini, Gondar Kusini, na maeneo ya Wag Hemra ambayo hapo awali yalikumbwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi. "Juhudi zinaendelea kufanywa ili kupunguza athari, lakini hatari bado ni ya kutisha," amesema Kamishna wa Tume ya Kikanda ya Kuzuia Maafa na Majanga ya Kimaumbile ya Ethiopia. 

Mamlaka husika katika jimbo lal Amhara zimekuwa katika hali ya tahadhari kufuatia indhari zilizotolewa na Taasisi ya Hali ya Hewa ya Ethiopia kuhusu hatari kubwa ya maporomoko ya ardhi kutokana na mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha. 

Mwezi uliopita, maporomoko mtawalia ya udongo yaliyouathiri ukanda wa Gofa kusini mwa Ethiopia yaliuwa watu takriban  260 na kulazimisha wengine 15,000 kuhama makazi yao.

Maporomoko ya udongo katika ukanda wa Gofa, Ethiopia mwezi uliopita

 

Tags