Jul 20, 2016 08:02 UTC
  • Tahadhari ya UN juu ya kupenya wanachama wa Daesh Afrika

Hivi karibuni Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, aliwasilisha ripoti ya siri mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na hatari ya kuenea kwa ugaidi, kupenya kwa kundi la Daesh (ISIS) na makundi mengine ya kigaidi kutoka nje ndani ya Libya na nchi nyingine za Afrika.

Katika ripoti hiyo, Ban Ki-moon alisema kuwa, kushindwa kwa kundi hilo huko Libya, kunaweza kuwafanya wanachama wake kuasisi kundi jipya dogo ambalo kijografia litaenea zaidi nchini Libya na nchi zingine jirani na taifa hilo la kaskazini mwa Afrika. Aliongeza kuwa, kushindwa kwa gange hilo mjini Sirte ni jambo linalowezekana, lakini akaonya kuwa, suala hilo litawafanya wanachama wake kukimbilia maeneo ya kusini mwa nchi na hata Tunisia, magharibi mwa nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Ban Ki-moon magaidi wa Daesh ambao ni kati ya 2000 hadi 5000 raia wa Libya, Tunisia, Algeria, Misri, Mali, Morocco na Mauritania, wako mjini Sirte, Tripol na Darnah nchini Libya. Askari wa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya walianzisha operesheni kali zilizoitwa 'Al-Bunyaan Al-Marsus' kwa lengo la kuutwaa mji wa Sirte ambao umekuwa ukidhibitiwa kwa muda sasa na wanachama wa kundi hilo. Kwa mujibu wa ripoti ya komandi ya operesheni hizo, kusonga mbele kwa askari wa serikali ya Libya kumetokea baada ya kujiri mapigano makali na magaidi wa Daesh (ISIS) hapo siku ya Ijumaa katika eneo la Ouagadougou, ambalo ndiyo ngome kuu ya kundi hilo mjini hapo Sirte. Tangu zilipoanza operesheni hizo hadi sasa zaidi ya watu 260 wakiwemo askari wa serikali ya umoja wa kitaifa wameuawa na wengine zaidi ya 1400 kujeruhiwa. Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa imefafanua kuwa, makumi ya magaidi wa kigeni ambao wanakimbia kutoka Libya na kuelekea Tunisia wanakusudia kutekeleza shambulizi nchi humo. Katika miezi ya hivi karibuni na katika operesheni tofauti, askari wa usalama wa Tunisia wamefanikiwa pakubwa kunasa idadi kubwa ya magaidi na makundi yenye mafungamano na kundi la Daesh. Wiki iliyopita, Wizara ya Mambo ya Ndani nchini Tunisia ilitangaza habari ya kunasa na kusambaratisha kundi moja la kigaidi katika maeneo ya mji wa Tunis, ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti ya wizara hiyo, baada ya kuwasaili magaidi hao, baadhi walikiri  kula kiapo na kutangaza utiifu wao kwa kundi hilo maarufu kwa kutenda jinai na kwamba walikuwa tayari kujiunga nalo. Katika fremu hiyo, hivi karibuni pia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Morocco ilitangaza kusambaratisha kundi la wanamgambo lenye mafungamano na genge hilo la kigaidi na kitakfiri Daesh. Upenyaji wa makundi ya kigaidi mbali na Daesh katika maeneo mengine ya nchi za Afrika bado unaendelea. Hivi sasa kundi la kigaidi la Boko Haram linaendeleza mashambulizi katika eneo la magharibi mwa Afrika hususan Nigeria na nchi nyingine za jirani na taifa hilo. Upande wa mashariki mwa Afrika, mapambano ya askari wa serikali ya Somalia kwa kushirikiana na askari wa kimataifa dhidi ya wanachama wa kundi la kigaidi la ash-Shabab, yangali yanaendelea. Aidha mapambano dhidi ya ugaidi, ni ajenda muhimu ya viongozi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kikao cha mwaka huu mjini Kigali, Rwanda. Katika kikao hicho, viongozi wa nchi za Kiafrika wametaka kutengwa bajeti maalumu kwa ajili ya kupambana na janga hilo la ugaidi. Rais Idriss Déby wa Chad ambaye anashikilia uenyekiti wa kiduru wa Umoja wa Afrika amewataka viongozi wa nchi za Afrika walioshiriki kikao hicho mjini Kigali, kulipa kipaumbele suala la mapambano dhidi ya ugaidi. Alisema kuwa kuwepo kwa mfuko kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugaidi ni suala la dharura sana na kwamba bajeti yake inatakiwa kudhaminiwa na nchi zenyewe za Kiafrika na waungaji mkono wa umoja huo.

Tags