Sep 18, 2024 11:30 UTC
  • HRW: Makundi yenye silaha yanatekeleza mauaji Burkina Faso

Shirika la Human Rights Watch (HRW) limesema kuwa makundi yanayobeba silaha yene mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida na kundi la kitakfiri la Daesh (ISIS) yamezidisha mashambulizi dhidi ya raia nchini Burkina Faso.

Ripoti iliyotolewa leo na shirika la Human Right Watch imeweka wazi kuhusu mauaji ya raia wasiopungua 128 katika mashambulizi saba yaliyofanywa na makundi yenye silaha huko Burkina Faso tangu mwezi Februari mwaka huu. HRW imesema kuwa, mauaji hayo ya raia ni kinyume na sheria ya binadamu ya kimataifa na ni jinai za kivita. 

Ripoti ya shirika la Human Right Watch imeeleza kuwa, makundi hayo yenye silaha yamekuwa yakiwauwa kwa umati wanavijiji na kuwalazimisha raia wengi kuwa wakimbizi.

Burkina Faso ambayo inaongozwa na serikali ya kijeshi ya Ibrahim Traore, imekuwa ikisumbuliwa na makundi ya wanamgambo wenye silaha kama mtandao wa kigaidi wa al Qaida na kundi la wanamgambo la JNIM tangu yalipohamia nchini humo mwaka 2016 yakitokea katika nchi jirani ya Mali. 

Ibrahim Traore, mtawala wa kijeshi wa Burkina Faso 

Kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso amewatolea wito wananchi kuchukua jukumu la kukabiliana na makundi hayo yenye silaha.

Shirika la HRW limesema kuwa kundi la wanamgambo la JNIM limehusika katika mashambulizi sita likiwemo shambulio la mwezi Juni katika kambi ya jeshi karibu na Niger ambapo wanajeshi 107 na raia wasiopungua 20 waliuawa.  

Tags