Guterres asikitishwa pakubwa na hali ya mambo ya al Fasher; Sudan
(last modified Sun, 22 Sep 2024 07:54:53 GMT )
Sep 22, 2024 07:54 UTC
  • Guterres asikitishwa pakubwa na hali ya mambo ya al Fasher; Sudan

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa "amesikitishwa sana" na ripoti za mashambulizi makubwa yaliyofanywa na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika mji wa al Fasher, makao makuu ya Jimbo la Darfur, Kaskazini mwa Sudan. Haya yameelezwa na Msemaji wa Antonio Guterres, Stephane Dujarric.

Dujarric amesema kuwa, Guterres amemtaka Luteni Jenerali Mohamed Hamdan 'Hemedti' Dagalo kuchukua hatua na kusitisha mara moja mashambulizi ya wapiganaji wake.

Wapiganaji wa kikosi cha RSF

"Ni jambo lisiloeleweka kwamba pande zinazozozana huko Sudan zimepuuza mara kwa mara wito wa kusitisha uhasama", amesema Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Amesisitiza kuwa usitishaji mapigano "si lazima tu, bali ni jambo la dharura huko al Fasher na katika maeneo mengine yote yenye migogoro huko Sudan. Hali ya kibinadamu katika mji wa al Fasher ni ya maafa; ambapo mamia ya maelfu ya watu wanahitaji misaada ya dharura."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemkumbusha Mjumbe wake Maalum, Ramtane Lamamra, kwamba aendelee na jitihada zake za kusaka amani huko Sudan. Antonio Guterers amesema kuwa yuko tayari kuunga mkono juhudi za kweli za kukomesha mapigano na kurejesha amani huko Sudan.