Maiti 13 za wahajiri zapatikana pwani ya kusini mashariki mwa Tunisia
Askari wa gadi ya baharini ya Tunisia wameopoa majini miili 13 ya wahamiaji wasio na vibali katika mkoa wa pwani wa Mahdia kusini mashariki mwa Tunisia.
Idhaa ya Tunisia ya Mosaique FM iliripoti habari hiyo jana Jumatano na kuongeza kuwa:"Miili kumi ilisukumwa hadi ufukweni Jumanne usiku huko Salakta, na nyingine tatu ilipatikana Chebba."
Farid Ben Jha, msemaji wa mahakama ya Mahdia na Monastir ameongeza kuwa, waliofariki dunia walikuwa wahamiaji kutoka nchi za Afrika Kusini mwa nchi za eneo la Jangwa la Sahara.
Ameeleza kuwa, miili hiyo 13 iliyokuwa imeharibika, ilihamishiwa hospitalini kwa ajili ya taratibu muhimu za kubaini utambulisho wao. Ben Jha ameongeza kuwa, uchunguzi umeanzishwa ili kubaini kiini hasa cha vifo hivyo.
Tunisia ambayo iko kwenye eneo la katikati mwa Bahari ya Mediterania, ni moja ya njia kuu zinazotumiwa na wahamiaji haramu wenye tamaa ya kufika barani Ulaya.
Mwaka jana 2023, Tunisia iliwakamata zaidi ya wahamiaji haramu 75,000 walipokuwa wanajaribu kuingia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania na wengi wao ni wale waliokuwa wanaelekea Italia.