Haaretz: Gaza imeharibiwa zaidi kuliko Hiroshima
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128708-haaretz_gaza_imeharibiwa_zaidi_kuliko_hiroshima
Katika ripoti ya kushtua iliyotegemea simulizi, picha za satelaiti na takwimu za Umoja wa Mataifa, gazeti la Israel limetangaza kuwa Gaza imeharibiwa zaidi kuliko miji ya Hiroshima na Nagasaki baada ya mashambulizi ya mabomu ya atomiki ya Marekani dhidi ya Japan.
(last modified 2025-07-24T08:38:57+00:00 )
Jul 24, 2025 08:38 UTC
  • Haaretz: Gaza imeharibiwa zaidi kuliko Hiroshima

Katika ripoti ya kushtua iliyotegemea simulizi, picha za satelaiti na takwimu za Umoja wa Mataifa, gazeti la Israel limetangaza kuwa Gaza imeharibiwa zaidi kuliko miji ya Hiroshima na Nagasaki baada ya mashambulizi ya mabomu ya atomiki ya Marekani dhidi ya Japan.

Mwandishi na mchambuzi wa Israel, Nir Hasson ameandika katika gazeti la lugha ya Kiebrania la Haaretz kwamba: "Tangu mwishoni mwa juma lililopita, hali ya njaa katika Ukanda wa Gaza imeongezeka sana na kwamba hospitali, mashirika ya misaada ya kibinadamu, waandishi wa habari na wakazi wenyewe wa Gaza wanaripoti uhaba mkubwa wa chakula ambao ni mbaya zaidi kuliko miezi iliyopita."

Siku ya Jumanne pekee, Wizara ya Afya ya Gaza ilitangaza kuwa watu 15 wamekufa kwa njaa na utapiamlo katika muda wa saa 24, wakiwemo watoto wanne. 

Gazeti la Haaretz limendelea kuripoti kuwa: "Njaa huko Gaza haionekani tu katika takwimu, lakini pia katika picha, video na simulizi chungu za watu: watoto waliodhoofika na matumbo yaliyovimba, ajuza wanaokula majani ya mtini na mama wasioweza kunyonyesha watoto wao."

Gaza

Haaretz limeandika kwamba kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na Umoja wa Mataifa, karibu theluthi moja ya majengo katika Ukanda wa Gaza, yameharibiwa.

Ripoti hiyo imesema, mbali na majengo ya makazi ya raia, jeshi la Israel limeharibu mamia ya hospitali, viwanda, misikiti, makanisa, masoko na vituo vya biashara. Vituo 2,300 vya elimu vimeshambuliwa na Israel, ambapo shule 501 kati ya jumla ya shule 564 za Ukanda wa Gaza zimeharibiwa.