Bunge la Afrika Mashariki lamuenzi Hafsa Mossi
(last modified Thu, 21 Jul 2016 13:52:13 GMT )
Jul 21, 2016 13:52 UTC
  • Bunge la Afrika Mashariki lamuenzi Hafsa Mossi

Bunge la Afrika Mashariki EALA limefanya kikao maalumu asubuhi ya leo mjini Arusha Tanzania, kwa ajili ya kumuenzi Hafsa Mossi, mwakilishi wa Burundi katika bunge hilo la kieneo ambaye aliuawa wiki jana mjini Bujumbura.

EALA imeanzisha mjadala juu ya kuanzisha wakfu wa kumkumbuka mwanasiasa na mwanadiplomasia huyo, ambaye wakati mmoja alikuwa Waziri wa Burundi katika masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.

Marehemu Hafsa Mossi

 

Akihutubia bunge hilo, Mike Sebalu, mwakilishi wa Uganda katika bunge la EALA amesema huu sio wakati wa kuomboleza kifo cha Hafsa Mossi, bali ni wakati wa kusherehekea maisha ya kujituma ya mwanasiasa huyo na kwamba bunge hilo la kieneo linatathmini jambo la kuanzisha ili kumbukumbu yake isifutike.

Hafsa Mossi aliuawa karibu na nyumba yake mjini Bujumbura kwa kufyatuliwa risasi mbili na watu wasiojulikana Julai 13. Marehemu ambaye pia alikuwa mwandishi wa habari mtajika, aliuawa baada ya kushuka kwenye gari lake kwenda kutizama gari lenye vioo vyeusi lililokuwa limegonga gari lake kutoka nyuma.

Tags