Jumuiya za kutetea haki za binadamu zataka sakata la kubakwa "binti" huko Tanzania lishughulikiwe ipasavyo
(last modified 2024-08-10T07:29:20+00:00 )
Aug 10, 2024 07:29 UTC
  • Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga
    Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yameendelea kupaza sauti yakitaka hatua za haraka zichukuliwe kuwashughulikia ipasavyo waliohusika na kitendo kiovu cha kumbaka na kumlawili binti mmoja wakidai kuwa wametumwa na "afande" kufanya ukatili huo.

Tukio hilo lilifichuliwa kwa mara ya kwanza kwa umma na Boniface Jacob, aliyekuwa Meya wa Ubungo, huko Dar es Salaam, Agosti 4 kupitia mtandao wa kijamii wa X. Jacob alidai kuwa wahusika wa ukatili huo wanaweza kuwa na uhusiano na jeshi la Tanzania, ingawa madai hayo hayajathibitishwa.

Baada ya kukaa kimya kwa siku kadhaa, Polisi ya Tanzania imetangaza kuwa imewakamata washukiwa wanne kati ya sita waliopanga na kutekeleza uhalifu huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Tanzania, video ya tukio hilo ilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii tarehe 2 Agosti mwaka huu ikiwaonyesha vijana watano wakimbaka na kumlawiti msichana mmoja na kudai kuwa wametumwa na afande. 

Polisi ya Tanzania imesema, tukio hilo lilifanyika Mei mwaka huu katika eneo la Swaswa jijini Dodoma. 

Chama cha Wanasheria Tanganyika kimelaani tukio hilo, na kulitaja kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za kijamii. 

Shirika la Msichana Initiative linalojikita katika kutetea haki za wasichana nchini Tanzania pia limetaka kuchukuliwe hatua madhubuti dhidi ya kile lilichokitaja kuwa ni vitendo vya kikatili. Shirika hilo limelaani kitendo cha kuendelea kusambaza video hiyo mtandaoni, likisema kuwa linazidisha fedheha kwa mwathiriwa.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC) kimemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kukemea ukati huo hadharani kikitahadharisha kuwa kushindwa kushughulikiwa masuala hayo kunaweza kusababisha ongezeko la vitendo hivyo chini ya mwavuli wa matumizi mabaya ya madaraka.

Tags