Oct 06, 2024 11:44 UTC
  • Watunisia wapiga kura kumchagua Rais

Wananchi wa Tunisia leo Jumapili wameshiriki katika uchaguzi wa rais pasina upinzani mkali dhidi ya rais aliyeko madarakani, Kais Saied, ambaye anatazamiwa kuibuka mshindi.

Uchaguzi huo wa Rais umefanyika leo Tunisia huku wakosoaji wakuu wa Rais Kais, akiwemo hasimu wake mkuu, wakiwa gerezani.

Nchi hiyo ya Afrika Kaskazini, kwa zaidi ya muongo mmoja sasa inajivunia kuwa kitovu cha vuguvugu la mapinduzi katika nchi kadhaa za Kiarabu yaliyopewa jina la  "Arab Spring".

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema asubuhi saa mbili na kufungwa saa kumi na mbili kwa wakati wa Tunisia. Tume ya Uchaguzi ya Tunisia imeeleza kuwa, matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais yanapasa kutangazwa kabla ya kesho Jumatano lakini yanaweza kujulikana mapema zaidi. 

Kabla ya wananchi wa Tunisia kuelekea katika masanduku ya kura, hakukuwa na mikutano ya kampeni au mijadala ya hadhara, na takriban mabango yote ya kampeni katika mitaa ya jiji la Tunisia ni ya Kais Saied. 

Kais Saied

Baada ya kuingia madarakani mwaka wa 2019, Saied, ambaye sasa ana umri wa miaka 66 na ambaye anaungwa mkono na tabaka la wafanyakazi, aliongoza na kusimamia mpango wa kuandika upya katiba ya Tunisia.

Hata hivyo mahasimu wake kadhaa wa kisiasa wamefungwa jela; hatua iliyoibua upinzani wa ndani na kutoka nje. Rached Ghannouchi mkuu wa chama cha An Nahdha cha Tunisia ambacho kilikuwa na uungaji mkono mkubwa wa kisiasa baada ya mapinduzi, ni miongoni mwa shakhsia wa kisiasa walioko jela. 

Al Ghannouchi, mwenye umri wa miaka 82 ambaye alikuwa spika wa bunge la Tunisia kabla ya kuvunjwa na Rais Saied mnamo Julai 2021, alikamatwa tareje 17 mwezi wa Aprili mwaka huu jana, na tangu wakati huo amekuwa akishikiliwa kizuizini kwa tuhuma za kupanga njama dhidi ya usalama wa nchi.

Mwanasiasa mwingine aliyeko jela ni Abir Moussi, mkuu wa chama cha Free Destourian ambacho wakosoaji wanakituhumu kuwa kilikuwa kikifanya juhudi za kuurejesha mamlakani utawala uliong'olewa madarakani huko Tunisia mwaka 2011. 

Tags