Oct 08, 2024 11:46 UTC
  • Wanaharakati Malawi waitaka serikali isiunge mkono jinai za Israel Gaza

Mashirika ya kiraia nchini Malawi yameiomba serikali ya Lilongwe kutazama upya msimamo wake kuhusu vita vya Israel huko Gaza "kwa sababu mtazamo na msimamo wake wa sasa ni kinyume na maadili yake ya amani na heshima kwa ubinadamu."

Assaboni Phiri, Mratibu Taifa wa Harakati ya Malawi ya Mshikamano na Palestina (MPSM) amesema msimamo wa sasa wa taifa hilo la kusini mwa Afrika unadhihirisha wazi kwamba, Lilongwe inaunga mkono kikamilifu mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel (huko Gaza).

"Malawi imesaini hati kadhaa za amani na kwa muda wote tumethamini amani na kutilia mkazo mazungumzo wakati wowote kunapotokea migogoro, lakini inasikitisha sana kwamba nchi hii imekhitari kuiunga mkono Israel tangu vita vilipoanza, bila kujali mateso ya wanawake na watoto huko Gaza. Huku ni kuondoka kabisa kwenye msimamo wetu juu ya amani na heshima kwa binadamu,” Phiri amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Malawi, Lilongwe.

Matamshi ya Phiri yamekuja sambamba na kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa vita vya mauaji ya halaiki ya Israel kwenye eneo la Palestina, ambavyo vimeua karibu watu 42,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Amebainisha kuwa, “Baada ya kupita mwaka mmoja, ulikuwa wakati muafaka wa kubadili msimamo wetu kwa kuzingatia kiwango cha uharibifu ambao vita vimesababisha maisha ya wanadamu. Tunapaswa kuacha kuisaidia Israel katika harakati zake za kufanya mauaji ya halaiki huko Gaza."

Naye Abdul Aziz Yasin, mchambuzi wa masuala ya kijamii nchini Malawi ameeleza bayana kuwa, "Kwa sababu ya kukata tamaa, tumepoteza maadili yetu kama taifa kwa sababu hatuna kile kinachohitajika ili kujisimamia."

Tags