Wabotswana wapiga kura huku chama kilichotawala kwa miaka 58 kikiahidi 'mabadiliko'
(last modified Wed, 30 Oct 2024 12:38:45 GMT )
Oct 30, 2024 12:38 UTC
  • Wabotswana wapiga kura huku chama kilichotawala kwa miaka 58 kikiahidi 'mabadiliko'

Wabotswana leo wameelekea kwenye vituo vya kupigia kura kuchagua wabunge watakaomchagua rais, wakati chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) ambacho kimeiongoza nchi hiyo kwa miaka 58 kikitafuta ridhaa tena ya kubaki madarakani kwa muhula mwingine wa miaka mitano kwa kaulimbiu ya kuleta "mabadiliko".

BDP ni miongoni mwa vyama tawala vilivyodumu kwa muda mrefu barani Afrika, kikiwa kinaiongoza Botswana tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1966.

Uchaguzi huo wa leo unafanyika huku Rais aliyeko madarakani Mokgweetsi Masisi, mwalimu wa zamani wa skuli ya sekondari na mfanyakazi wa zamani wa shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF aliye na umri wa miaka 63, akiwa na matumaini ya kuiongoza tena Botswana kwa muhula wa pili na wa mwisho.

Mokgweetsi Masisi

Botswana yenye idadi ya watu wapatao milioni mbili na nusu imekuwa ikitajwa kwa muda mrefu kama mfano wa mafanikio katika eneo la kusini mwa Afrika kwa siasa na uchumi wake uliotulia, lakini kushuka kwa mahitaji ya almasi duniani katika miaka ya hivi karibuni kumechangia kupanda kwa gharama za maisha na kusababisha ukosefu wa ajira kuongezeka hadi 27%.

Wabotswana wapatao milioni moja wametimiza masharti ya kupiga kura katika uchaguzi huo wa Bunge, ambapo rais Masisi Masisi amechuana na wapinzani wakuu watatu, ambao ni Duma Boko wa chama kikuu cha upinzani cha Umbrella for Democratic Change, Dumelang Saleshando wa Botswana Congress Party na Mephato Reatile kutoka Botswana Patriotic Front.

Ingawa wachambuzi wanasema matokeo ya uchaguzi ni magumu kutabiri mara hii, lakini BDP imeshashinda kwa kupata wabunge wengi katika chaguzi zote 11 zilizofanyika nchini humo tangu uhuru.../

 

Tags