Obasanjo: Demokrasia ya magharibi haifai tena barani Afrika
Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ameitaka nchi yake kufikiria kupitisha mfumo wa serikali unaozingatia kanuni za kitamaduni za Kiafrika, akisisitiza kuwa demokrasia ya Magharibi imeshindwa barani humo.
Obasanjo alitoa kauli hiyo katika hafla ya kumuaga makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Chrisland anayemaliza muda wake, Chinedum Babalola, katika Jimbo la Ogun kusini magharibi.
Rais huyo wa zamani wa Nigeria amenukuliwa akisema: "Siku zote nimekuwa nikizungumza kuhusu demokrasia ya kiliberali ya Magharibi. Haifanyi kazi kwetu. Haifanyi kazi hata kwa wale waliotupa. Waingereza walikuwa wakilalamika. Ni lazima tufikirie upya demokrasia."
Obasanjo amesisitiza kuwa: "Lazima tulete utamaduni wetu katika demokrasia. Utamaduni wa Kiafrika hauzungumzii upinzani; bali unazungumza kuhusu ujamaa; mnakutana, kujadiliana, kusuluhisha, halafu mnafanya kazi pamoja".
Novemba mwaka jana, rais huyo wa zamani alitoa mwito sawa na huo katika mkutano wa ‘Kufikiri Upya Demokrasia ya Kiliberali ya Magharibi barani Afrika’, akieleza kuwa muundo wa kisiasa uliwekwa na madola ya kikoloni na hivyo kushindwa kufanya kazi ipasavyo barani Afrika.
Bara la Afrika limekumbwa na msukosuko wa kisiasa katika miaka ya hivi karibuni, uliochochewa na mapinduzi ya kijeshi kufuatia kushindwa kwa viongozi waliochaguliwa kwa mtindo wa demokrasia ya Magharibi.