Somaliland yajitoa kimasomaso, yakanusha kuafiki kujengwa kambi za kijeshi za Israel
Eneo la Somaliland la kaskazini mwa Somalia limekanusha madai kwamba lilikubali kuwa mwenyeji wa vituo vya kijeshi vya Israel na kuwapokea Wapalestina waliofurushwa kutoka Gaza ili kutambuliwa na Israel.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Somaliland jana Alkhamisi ilipuuzilia mbali madai hayo na kusisitiza kuwa hayana msingi, ikisema ushirikiano wake na Israel ulikuwa "wa kidiplomasia tu" na uliendeshwa "kwa heshima kamili ya sheria za kimataifa".
Taarifa hiyo imekuja kujibu madai ya Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, ambaye aliiambia Al-Jazeera kwamba, Somaliland imekubali masharti matatu kutoka kwa Israel: Kuwapa Wapalestina makazi mapya, kuanzishwa kwa kituo cha kijeshi kwenye pwani ya Ghuba ya Aden, na kujiunga na Mkataba wa Abraham ili kuufanya wa kawaida uhusiano wake na Israel.
Ripoti zilianza kusambaa mapema mwaka uliomalizika kwamba Somaliland ilikuwa na nia ya kusaidia lengo la Israel lililolaaniwa sana la kuwaangamiza Wapalestina, huku maafisa wa Hargeisa wakiendelea kushinikiza kutambuliwa kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somaliland amesema hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika kuhusu suala hilo, lakini hakupinga kuwepo uwezekano huo, tofauti na nchi nyingine zinazodaiwa kuwa na maslahi kwa Israel.
Hii ni katika hali ambayo maelfu ya wananchi wa Somalia wameendelea kumiminika mabarabarani katika miji mbali mbali ya nchi hiyo, kupinga na kulaani uamuzi wa utawala haramu wa Israel wa kulitambua eneo la Somaliland la kama taifa huru.
Hali kadhalika utawala wa Kizayuni wa Israel umeendelea kulaaniwa kote duniani kwa kulitambua eneo hilo lililotangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991.