Safaricom yajitetea, yasema haitoi data za wateja kwa maafisa usalama
Kampuni ya mawasiliano ya Safaricom nchini Kenya hatimaye imekiri hutumia programu ya kampuni ya Neutral Technologies inayodaiwa kutumiwa na kampuni za mawasiliano kutoa data za kibinafsi ili kusaidia polisi kuendeleza utekaji nyara.
Hata hivyo, kampuni hiyo imefafanua kuwa hutumia programu hiyo kufanikisha usakaji wa walaghai wa kifedha pekee.
Taarifa iliyotolewa na kampuni ya Safaricom imesema kwamba: “Kampuni ya Neutral Technologies inayo sifa kimataifa na huendesha shughuli zake katika zaidi ya nchini 30 kusaidia kampuni za mawasiliano kugundua na kuzuia ulaghai wa kifedha. Hii ndio maana mnamo 2012 Safaricom ilikodi Neutral Technologies kutekeleza mfumo wa kudhibiti ulaghai wa kifedha katika laini zetu zote.”
Safaricom imeongeza kuwa: “Hata hivyo, programu hii haitumiki kufanikisha utoaji wa data au maelezo ya wateja wetu kwa watu wengine, wakiwemo maafisa wa usalama.”
Safaricom imetoa ufafanuzi huo kufuatia ripoti maalumu iliyochapishwa katika gazeti la Daily Nation, toleo la Oktoba 29, 2024 ambapo ililaumiwa kwa kutoa data za wateja wake kwa polisi kufanikisha utekaji nyara.
Ripoti hiyo maalumu ilichapishwa kufuatia uchunguzi wa wanahabari kwa kipindi cha mwezi mmoja, ambayo inaanika jinsi polisi wamekuwa wakipata data za mawasiliano ya simu za wateja wa kampuni za mawasiliano na kuzitumia kuwateka nyara watu wanaosawiriwa kuwa wakosoaji wa serikali.
Baadhi ya wanaotekwa nyara hupatikana wameuawa na miili yao kutupwa kwenye misitu au kando mwa mito.