Chama tawala Botswana chabwagwa baada ya kuongoza kwa karibu miongo 6
Chama tawala cha Botswana Democratic Party (BDP) ambacho kimeiongoza nchi hiyo kwa miaka 58, kimebwagwa vibaya katika uchaguzi wa Bunge uliofanyika Jumatano ya juzi Oktoba 30.
Tayari Rais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi amekubali kushindwa huku matokeo ya awali yakionyesha kuwa, chama chake kimepoteza wingi wa wabunge baada ya takriban miongo sita madarakani. Wabunge ndio humchagua rais nchini Botswana.
Hatua ya leo Ijumaa ya Masisi kunyanyua mikono juu imekuja kabla ya matokeo ya mwisho kutangazwa, huku chama chake cha BDP kikishika nafasi ya nne, kwa mujibu wa matokeo ya awali ya Tume Huru ya Uchaguzi.
Rais Masisi ambaye alikuwa akitafuta muhula wa pili wa miaka mitano katika uchaguzi wa Jumatano, ametangaza kuwa "amejiondoa" baada ya chama chake kupigishwa mweleka.
BDP ilimteua Rais Mokgweetsi Eric Masisi, 63, katika kinyang'anyiro hicho, na ujumlishaji wa matokeo yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi unaonyesha kuwa, vyama vya upinzani vimeshinda angalau viti 35 kati ya 61 katika Bunge. Masisi amehudumu kwa muhula mmoja tu, baada ya kurithi mikoba ya Ian Khama mwaka wa 2019.
Chama kikuu cha upinzani cha Umbrella for Democratic Change (UDC) kimeongoza kwa kiasi kikubwa katika matokeo hayo ya muda, na kumfanya kiongozi wake, Duma Boko, kuwa katika mkondo wa kuwa rais mpya wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika askishapata ridhaa ya Bunge.