Chad inawapa hifadhi wakimbizi zaidi ya 680,000 wa Sudan
(last modified Sat, 09 Nov 2024 06:35:01 GMT )
Nov 09, 2024 06:35 UTC
  • Chad inawapa hifadhi  wakimbizi zaidi ya  680,000 wa Sudan

Zaidi ya wakimbizi 680,000 wa Sudan wamepata mazingira salama nchini Chad, baada ya kulazimika kukimbia vita vinavyoendelea nchini Sudan.

Hayo yameelezwa na Filippo Grand Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR na kubainisha kuwa mwezi uliopita, wakimbizi wapya wapatao  60,000 waliwasili nchini Chad.

Idadi kubwa ya waliowasili ni wanawake na watoto, na wengi wanafika mpakani baada ya kutembea masafa marefu kabla ya kuingia katika nchi hiyo jirani ya Chad.

Mmoja wa wakimbizi hao amesema: "hatukuwa na chakula nyumbani, sehemu ya nyumba yangu ilichomwa moto. Kabla hatujaondoka nchini Sudan, watu saba waliuawa mbele ya nyumba yetu. Usiku umekuwa wa kutisha kwetu, kuna watu wengi ambao wameuawa. Nilipoteza mali zangu zote za thamani. Hapo awali, hatukuishi El-Geneina. Tulikuwa kilomita chache kutoka El-Geneina ambako tulifuga ng’ombe, mbuzi, na kuku.  Tumepoteza kila kitu tulichokuwa nacho".

Hata hivyo, mateso ya wakimbizi kutoka Sudan  hayaishi baada ya kuwasili nchini  Chad. Wakimbizi hao wanafikia katika nchi yenye rasilimali chache. Kulingana na takwimu za  Umoja wa Mataifa, Chad sasa hivi inakabiliwa na wimbi kubwa la wakimbizi kuwahi kushuhudiwa katika historia yake.

Uchumi dhaifu wa nchi hiyo na miundombinu yake duni vinakabiliwa na mchanganyiko wa mgogoro, athari hasi za tabianchi na uhaba wa chakula.

Grandi ameendelea kueleza: "katika muktadha wa hali mbaya za kibinadamu zisizoisha, misaada haba ya fedha za misaada ya kibinadamu, na wakati upokeaji wa watu waliolazimika kuhama makwao unaiathiri sana jamii ya wenyeji wanaowapokea, tunahitaji kutafakari upya mbinu zetu za uhamishaji wa wakimbizi ili kuzifanya ziwe endelevu zaidi.