Baraza la Usalama kuzichukulia hatua pande hasimu nchini Sudan
(last modified Tue, 12 Nov 2024 12:46:55 GMT )
Nov 12, 2024 12:46 UTC
  • Baraza la Usalama kuzichukulia hatua pande hasimu nchini Sudan

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamesema kuwa, wanathathmini azimio lililoandaliwa na Uingereza, kutaka jeshi na wanamgambo wa RSF nchini Sudan, kusitisha mapigano na kuruhusu misaada ya kibindamu kuwafikia mamilioni ya watu walioathiriwa na mzozo huo.

Azimio hilo linahitaji kuungwa mkono kwa kura tisa bila ya kuwepo kwa kura ya turufu kutoka wajumbe wa kudumu ambao ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Russia na China. Uingereza inataka azimio hilo kupigiwa kura haraka iwezekanavyo.

Hii ni katika hali ambayo, huko nyuma Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha maazimio mawili ya awali kuhusu Sudan mwezi Machi na kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa uhasama wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Haya yanajiri wakati huu, ikiwa ni mara ya kwanza kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa kuzuru mji wa Port Sudan, kwa siku tatu, kujionea hali ilivyo hasa kwenye jimbo la Darfur.

Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, karibu watu milioni 25, nusu ya wakazi wa Sudan wanahitaji msaada huku njaa ikishuhudiwa katika kambi za wakimbizi na watu milioni 11 wamekimbia makazi yao. Karibu watu milioni 3 wamelazimika kuwa wakimbizi nje ya nchi.