Kuimarishwa uhusiano wa kiusalama kati ya Iran na Pakistan
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kuwa katika safari yake ya hivi karibuni nchini Pakistan, ameshauriana na viongozi wa kijeshi na kisiasa wa nchi hiyo kuhusiana na namna ya kukabiliana na ugaidi, ambayo ni changamoto kubwa zaidi katika eneo.
Sayyid Abbas Araghchi, aliwasili Islamabad, mji mkuu wa Pakistan Jumatatu iliyopita kwa lengo la kukutana na kushauriana na viongozi wa ngazi za juu wa Pakistan kuhusu uhusiano wa pande mbili na matukio ya eneo. Katika mazungumzo hayo, pande mbili ziliamua kuimarisha hatua za pamoja za kukabiliana na ugaidi katika pande zote za mpaka wa pamoja.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika mahojiano na kanali ya PTV World ya Pakistan kuhusu suala hilo kuwa, kwa kutilia maanani matukio yanayoendelea katika eneo na mashambulizi yanayofanywa na utawala katili wa Kizayuni huko Gaza na Lebanon, kuna uwezekano mkubwa wa kuenea vita katika eneo zima, hivyo ameitembelea Pakistan ili kujadiliana na viongozi wa nchi hiyo kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto hizo, likiwemo suala la ugaidi.
Kuna wasi wasi mkubwa katika duru za kieneo kwamba huenda jinai za utawala wa Kizayuni zikaenea na kuwa vita vya pande zote katika eneo. Moja ya njia muhimu za kukomesha mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika eneo ni kuanzisha uratibu na ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu za eneo. Hii ni kwa sababu licha ya kuwa nchi za Kiislamu zina uwezo mkubwa na kamili wa kuzuia jinai na ukatili wa utawala wa Kizayuni, lakini uwezo huo unapasa kuratibiwa na kuimarishwa kupitia ushirikiano wa nchi hizi kwa madhumuni ya kukabiliana na uungaji mkono wa Magharibi kwa utawala ghasibu wa Quds Tukufu huko Palestina.
Aidha katika safari ya Araghchi nchini Pakistan pande mbili zimejadiliana kuhusiana na namna ya kukabiliana na tatizo la ugaidi ambayo ni changamoto kubwa na hatari katika eneo, ili kuchukuliwa hatua madhubuti na za pamoja za kukabiliana na ugaidi katika pande zote za mipaka ya nchi mbili.
Makundi ya kigaidi, ikiwa ni pamoja na la Jaish al-Dhulm, yanahatarisha pakubwa usalama wa nchi hizi kwa kukimbia na kujificha katika maeneo ya mpaka wa pamoja wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan. Shambulio la hivi karibuni la kundi hilo la kigaidi katika ardhi ya Iran ambalo lilipelekea kuuawa shahidi askari kumi wa Iran, lilionyesha kuwa, Tehran na Pakistan zinapaswa kupanua zaidi ushirikiano wao wa kijeshi na kiusalama kuliko wakati mwingine wowote ili kukomesha maovu katika sehemu zote za mipaka ya pande mbili.
Katika fremu ya sera ya ujirani mwema, Iran na Pakistan zina uwezo wa kuinua kiwango cha ushirikiano wao, jambo ambalo linatoa ulazima wa kukabiliana na ugaidi na makundi yanayoibua ghasia na migogoro ya mara kwa mara katika eneo.
Ikumbukwe pia kwamba licha ya kuwa uhusiano wa Iran na Pakistan ni wa kihistoria na uanoendelea kukua, lakini hauridhishi katika nyanja kadhaa ukiwemo wa kiuchumi. Kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi, kiviwanda na kiteknolojia katika nchi zote mbili, Tehran na Islamabad,zinaendelea kufanya juhudi za kuuboresha na zina matumaini ya kufikia lengo la dola bilioni tano 5 katika mabadilishano ya bidhaa za kibiashara.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ingawa vikwazo vya kidhalimu vya nchi za Magharibi dhidi ya Iran bado vipo, lakini Tehran na Islamabad zina uwezo wa kupitisha stratijia na utaratibu mpya wa ushirikiano wa kiuchumi bila ya kujali vizingiti na vikwazo hivyo ili kuboresha uhusiano wa pande mbili.