Tunisia yasambaratisha mtandao wa magendo ya binadamu karibu na mji mkuu Tunis
(last modified Wed, 13 Nov 2024 02:18:43 GMT )
Nov 13, 2024 02:18 UTC
  • Tunisia yasambaratisha mtandao wa magendo ya binadamu karibu na mji mkuu Tunis

Walinzi wa Taifa wa Tunisia wametangaza kuwa wamesambaratisha mtandao wa magendo ya binadamu unaohusika na kusafirisha wahamiaji wasio na vibali na wamewatia mbaroni watu watano katika operesheni hiyo.

Operesheni hiyo imeendeshwa katika jimbo la Ben Arous karibu na mji mkuu Tunis baada ya kupatikana taarifa za kiintelijensia za kuweko mtandao unaosafirisha wahamiaji wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara la barani Afrika wasio na vibali.

Taarifa ya kikosi hicho maalumu cha Tunisia imesema: Wahamiaji hao walihamishwa kwa siri kutoka mkoa wa magharibi wa Kasserine na kupelekwa jimbo la kusini mashariki la Sfax, ambapo walikuwa wakisubiri kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea barani Ulaya.

Jeshi la Ulinzi la Taifa la Tunisia halikubainisha wazi muda wa operesheni hiyo wala uraia wa washukiwa hao lakini lilithibitisha kuwa wanne kati yao walikuwa tayari wakisakwa kwa tuhuma mbalimbali. Magari matano yalikamatwa wakati wa operesheni hiyo na washukiwa hao kwa sasa wako chini ya ulinzi, wakisubiri taratibu za kisheria.

Watoto wachanga kwenye mbeleko ni miongoni mwa wahanga wakubwa wa janga la magendo ya binadamu

 

Tunisia, iko kwenye ncha ya kaskazini mwa Afrika na inaendelea kuwa kituo kikuu cha uhamiaji haramu kuelekea barani Ulaya.

Katika operesheni tofauti, Walinzi wa Taifa wa Tunisia walikamata watu sita wakiwemo wanawake wawili katika jimbo la Sfax kwa kujihusisha na mtandao wa magendo ya dawa za kulevya.

Vikosi vya Tunisia vimekamata madawa ya kulevya aina ya kokeini, magari mawili yaliyotumika kusafirisha mihadarati hiyo na pesa taslimu. Watu waliokamatwa wamefikishwa kwenye mamlaka husika kwa taratibu za kisheria.