Waandishi habari Sudan wanatangatanga, vita vimewalazimisha wengine kuacha kazi
(last modified Sun, 17 Nov 2024 07:49:17 GMT )
Nov 17, 2024 07:49 UTC
  • Waandishi habari Sudan wanatangatanga, vita vimewalazimisha wengine kuacha kazi

Baada ya vita vya zaidi ya miezi 18 nchini Sudan kati ya jeshi la taifa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), hali ya wadau wa vyombo vya habari nchini humo imeendelea kuwa mbaya, na wengi wao wamepoteza ajira zao na baadhi yao wamelazimika kuingia kwenye nyanja nyingine kwa ajili ya kutafuta riziki.

Uchapishaji wa magazeti nchini Sudan umesitishwa na matangazo mengi huchapishwa kwenye mitandao ya kijamii tena aghlabu kupitia juhudi za watu binafsi.

Vita vya ndani huko Sudan vimeharibu taasisi za vyombo vya habari na miundombinu yao, na magazeti ya kuchapisha yamesimama kabisa ikiwa ni kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miaka 120, na kuacha karibu 90% ya wafanyakazi katika sekta hiyo bila kazi wala ajira. Vilevile "Redio ya Taifa ya Omdurman" imefungwa, suala ambalo halikuwahi kutokea tangu ilipoanzishwa mnamo 1940, ingawa imenza tena utangazaji hivi karibuni.

Waandishi wa habari wa ndani ya nchi huko Sudan wanasumbuliwa na kuyumba kwa mawasiliano na huduma za mtandao, na kukatwa huduma hizo wakati mwingine katika maeneo yenye migogoro, jambo ambalo linawazuia kutekeleza majukumu yao, na kutatiza kazi ya kufika kwenye vyanzo na kufikisha habari kwa raia, na hivyo kuwa sababu ya kuenea uvumi.

Katibu Mkuu wa zamani wa Baraza la Vyombo vya Habari na Machapisho nchi Sudan, Abdel-Azim Awad, anasema kuzorota kwa uandishi wa habari nchini kulianza mwishoni mwa enzi za rais aliyeng'olewa madarakani, Omar al-Bashir, na kuendelea katika utawala wa Waziri Mkuu wa zamani Abdullah Hamdok. Abdel-Azim Awad amesisitiza kuwa vita vya sasa "vimepiga risasi ya mwisho katika jeneza za sekta ya habari nchini Sudan."