'Ugonjwa usiojulikana' DRC wabainika kuwa ni Malaria sugu
(last modified Thu, 19 Dec 2024 06:59:41 GMT )
Dec 19, 2024 06:59 UTC
  • 'Ugonjwa usiojulikana' DRC wabainika kuwa ni Malaria sugu

Ugonjwa ambao haukutambuliwa hapo awali ambao ulizuka katika jimbo la Kwango kusini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umebainika kuwa ni aina sugu ya malaria.

Mapema mwezi huu, mamlaka ya eneo hilo iliripoti kwamba ugonjwa huo, ambao haukujulikana hapo awali, uliopelekea watu 143 kufariki mnamo Novemba. Dalili ni pamoja na homa, maumivu ya kichwa, kikohozi, mafua, na maumivu ya mwili.

Wizara ya Afya ya DRC imetangaza jana kwamba: "Siri hatimaye imetatuliwa: ni kisa cha malaria sugu inayojidhihirisha kama ugonjwa wa kupumua. Aidha wizara hiyo imesema utapiamlo katika eneo hilo umeshadidisha ugonjwa huo.  Taarifa hiyo imesema tangu Oktoba, kumekuwa na kesi 592 zilizoripotiwa na kiwango cha vifo cha 6.2%/

Wengi wa watu walioathirika ni watoto. Mlipuko huo umejikita zaidi katika maeneo tisa kati ya 30 ndani ya eneo la afya la Panzi, takriban kilomita 700 (maili 435) kutoka Kinshasa, jambo ambalo lilifanya uchunguzi na juhudi za kukabiliana nazo kuwa ngumu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetuma timu ya wataalamu katika eneo la Panzi kusaidia kutambua ugonjwa huo na kudhibiti mlipuko huo.

Wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alifichua kwamba sampuli kumi za awali za wagonjwa nchini DRC walioathiriwa na ugonjwa huo 'usiojulikana' zilipatikana na malaria. Hata hivyo, alisisitiza kuwa ugunduzi huu haukuondoa uwepo wa magonjwa mengine yanayotokea kwa wakati mmoja.

Waziri wa afya wa jimbo hilo, Apollinaire Yumba amewaambia waandishi wa habari kuwa mbinu za matibabu ya malaria zilizopendekezwa na WHO zinatumika katika hospitali na vituo vya afya katika eneo hilo.

Malaria, mojawapo ya magonjwa hatari zaidi ya kuambukiza duniani, huambukizwa na mbu. Inaweza kuchukua wiki kuonyesha dalili na kwa kawaida husababisha homa, kutapika, kuhisi baridi na dalili zinazofanana na mafua. Ingawa inatibika, malaria inasalia kuwa tishio kubwa katika nchi zinazoendelea, ambapo huchukua maisha ya watu 600,000 kila mwaka, 93% yao wakiwa barani Afrika.